Apple yaamrishwa kuifungua simu ya muuaji

Image caption Muuaji wa San Bernadinho Syed Farook

Jaji mmoja katika jimbo la Carlifonia nchini Marekani ameiamrisha kampuni kubwa ya Teknolojia ya Apple kusaidia polisi katika kuchunguza simu ya mwanamume ambaye aliwapiga risasi watu 14 katika eneo la San Bernardino mwezi Disemba.

Syed Rizwan Farook na mkewe waliuawa na polisi baada ya kisa hicho.

Jaji alisema kuwa kampuni ya Apple ni lazima itoe msaada wa kiteknolojia baada kushindwa kuweka nywila ya simu hiyo kwa mara kumi. . Kampuni hiyo bado haijatoa tamka lolote na ina muda wa siku tano kupinga uamuzi huo.

Tangu kutolewa kwa programu mnamo mwezi Septemba 2014,data ya simu za Apple kama vile ujumbe na picha zimewekewa usalama wa kutosha.

Hii ina maanisha kwamba iwapo simu hiyo imefungwa ,ni nywila au neno la siri la simu hiyo linaloweza kuifungua na kupata data hiyo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Simu ya Apple

Iwapo mtu atajaribu mara 10 bila mafanikio data iliopo ndani ya simu hiyo hujifuta .

Hakuna mtu ama hata kampuni ya Apple itaweza kupata ujumbe huo,hatua ambayo kampuni hiyo ilifanya kufuatia ufichuzi wa bwana Edward Snowden kwamba serikali ya Marekani imekuwa ikidukua simu za raia.