Wenye itikadi kali kujengewa jela maalum Kenya

Magereza
Image caption Rais Kenyatta amesema serikali itaangazia changamoto zinazokabili idara ya magereza

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema nchi hiyo itajenga jela mpya ya kuwazuiliwa wafungwa wenye itikadi kali.

Kiongozi huyo amesema hatua hiyo itazuia wafungwa hao kutoeneza itikadi hizo kwa wafungwa wengine.

Kwa sasa ni wafungwa waliohukumiwa kunyongwa pekee ambao hutengwa na wafungwa wengine gerezani nchini Kenya.

Magereza Kenya yamekabiliwa na msongamano mkubwa na maisha humo huwa magumu.

Askari jela pia wamelalamikia hali duni ya mazingira ya kufanyia kazi pamoja na malipo duni.

Rais Kenyatta alitangaza mpango huo akihutubu wakati wa hafla ya kufuzu kwa zaidi ya askari jela 2,000 Jumanne.

Amesema serikali yake imeanzisha mpango wa kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikikabili idara ya magereza.

Kenya imekabiliwa na tishio la wahalifu wenye itikadi kali, hasa kutoka kwa kundi la Kiislamu la al-Shabab kutoka Somalia.

Kundi hilo limekuwa likitekeleza mashambulio ya kigaidi mara kwa mara.

Wanajeshi karibu 4,000 wa Kenya wamo Somalia kusaidia kikosi cha Umoja wa Afrika kukabiliana na wanamgambo hao.