Polisi waahidi amani uchaguzini Uganda

Kale
Image caption Bw Kayihura amesema wapiga kura hawafai kuwa na wasiwasi

Mkuu wa polisi nchini Uganda ameahidi kwamba maafisa watakuwa macho kuhakikisha amani na utulivu wakati wa uchaguzi mkuu kesho.

Inspekta mkuu wa polisi Kalekezi Kayihura amesema wapiga kura hawafai kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wao.

Amesema kisa kilichotokea Jumatatu ambapo polisi walikabiliana na wafuasi wa mgombea urais wa upinzani Kizza Besigye kilitokana na kutoelewana na ukosefu wa ushirikiano.

Bw Besigye alizuiliwa na polisi kwa muda.

Polisi walisema alizuiliwa kwa sababu alikuwa akipitia maeneo yasiyoruhusiwa katika mji wa Kampala.

Mtu mmoja alifariki wakati wa makabiliano kati ya wafuasi wake na polisi yaliyodumu saa kadha.

"Tumekuwa na utulivu wakati huu wa kabla ya uchaguzi, isipokuwa visa kadha hapa na pale,” Bw Kayihura ameambia wanahabari mjini Kampala.

"Yaliyotokea Jumatatu yalitokana na ukosefu wa ushirikiano kutoka upande wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC) (chama chake Besigye). Jana kulikuwa na utulivu.”