Ajabu ya mwanamke kushika mimba jela Vietnam

Mwanamke Haki miliki ya picha Thinkstock
Image caption Inadaiwa mwanamke huyo alilipa $2,300

Askari jela wanne nchini Vietnam wamesimamishwa kazi kwa kosa la kuzembea kazini baada ya mfungwa wa kike aliyehukumiwa kunyongwa kushika mimba.

Wachunguzi wanasema Nguyen Thi Hue, 42, alijitungisha mimba kwa kutumia mbegu za kiume kutoka kwa mfungwa wa kiume, ili kukwepa hukumu ya kifo.

Sheria ya Vietnam inasema mwanamke mjamzito au mwenye mtoto wa chini ya umri wa miaka mitatu hawezi kunyongwa na badala yake hukumu yake inafaa kubadilishwa na kuwa kifungo cha maisha jela.

Sasa inatarajiwa kwamba hukumu yake itapunguzwa kutoka kifo hadi maisha jela kwa sababu atakuwa na mtoto wa chini ya miaka mitatu.

Maafisa wanasema Hue alinunua mbegu kutoka kwa mfungwa wa kiume wa umri wa miaka 27 kwa $2,300 (£1,600).

Mfungwa huyo alimpa mbegu zake mara mbili Agosti mwaka 2015.

Mwanamke huyo anatarajiwa kujifungua Aprili.

Kisa hicho kimetokea katika mkoa wa Quang Ninh, kaskazini mwa nchi hiyo ingawa polisi bado hawajakizungumzia.

Mwaka 2007, askari jela wawili katika mkoa wa Hoa Binh kaskazini mwa nchi hiyo walimruhusu mwanamke kushika mimba akiwa jela, kwa mujibu wa gazeti la Thanh Nien. Alikwepa kunyongwa.