Watu 71 wafariki katika ajali Ghana

Image caption Rais wa Ghana John Mahama

Takriban watu 71 wamefariki katika ajali mbaya ya barabarani kuwahi kufanyika nchini Ghana katika kipindi cha miaka mingi.

Basi moja lililokuwa limejaa abiria liligongana ana kwa ana na lori lililojaa tomato kaskazini mwa taifa hilo siku ya jumatano jioni.

Watu 58 walifariki papo hapo ,10 wakifariki katika hospitali ya Bismack Owusu huku 3 wakifariki katika hospitali nyengine ya karibu.

Rais wa Ghana John Mahama ameielezea ajali hiyo kama ''habari mbaya'' katika mtandao wake wa tweeter na kuongezea kuwa huduma ya kukabiliana na maswala ya dharura inakabiliana na hali hiyo.

Baadhi ya walionusurika wamewaambia polisi kwamba breki za lori hilo zilifeli ,lakini kiini cha ajali hiyo kinachunguzwa.

Hatahivyo kuna hasira na shutma katika mitandao ya kijamii baada ya picha za kuogofya za ajali hiyo kusambazwa.