Wasifu wa Kyalya, Mgombea urais mwanamke Uganda

Maureen Haki miliki ya picha Maureen Kyalya Facebook
Image caption Maureen Kyalya ana umri wa miaka 41

Maureen Faith Kyalya Waluube ni mwanawe marehemu Kanobe Kyalya, mwanachama sugu wa chama cha Democrtic Party ambaye alikuwa meya wa mji wa Jinja miaka ya 80.

Mamake Irene Wekiya wakati mmoja aliiwakilisha Jinja bungeni na sasa ni balozi wa Uganda katika nchi za Emirata.

Maureen ameolewa na ana watoto watatu.

Kyalya ambaye anajiita mwanaharakati wa mageuzi katika jamii, ni wakili aliyesomea katika chuo kikuu cha Portmouth nchini Uingereza.

Kwa elimu yake ya Upili alikwenda katika shule ya sekondari ya Iganga.

Maureen aliidhinishwa na tume ya uchaguzi, na kujiunga na wagombea urais wengine saba, wote wanaume.

Lakini yeye ni nani?

Mbali na jamii yake, Kyalya alikuwa hajulikani mjini Jinja licha ya kwamba aliwania kiti cha ubunge cha wilaya miongoni cha wanawake na karibu ashinde.

Kyalya alitumia wakati wake mwingi akiishi na kusoma nchini Uingereza, kwa hivyo ni watu wachache waliomjua katika jimbo la Busoga ambapo alizaliwa miaka 41 iliyopita.

Katika uchaguzi wa mwaka 2011, Kyalya aliushangaza mji wa Jinja,na kupata umaarufu wa haraka ambapo alionekana kama mgombea aliyekuwa kifua mbele katika kugombea kiti hicho cha wanawake.

Aliwania kiti hicho baada ya mamake Irene Wekiya kupoteza katika mchujo dhidi ya Nabiriye na kuamua kujiondoa katika kinyang'anyiro.

Kyalya ambaye alikuwa mgombea wa chama cha FDC alishindwa na Agnes Nabirye wa chama cha NRM.

Licha ya kuwa mgombea mpya katika kinyang'anyiro hicho cha kisiasa, Kyalya alifanya kampeni kali na kuwavutia wapiga kura wengi.

Alipinga matokeo ya uchaguzi huo mahakamani kabla ya uamuzi kutolewa, lakini aliwashangaza wafuasi wake aliposema amepoteza hamu ya kesi hiyo.

Mwaka 2012 mwezi Julai, alichaguliwa kama mshirikishi wa kitaifa wa mpango wa kuondoa umaskini katika kata ndogo ya jimbo la Busoga, akifanya kazi kwa ushirikiano na ikulu ya rais.

''Sababu iliyonifanya kujiunga na siasa ilikuwa kupiga vita ufukara miongoni mwa wakaazi wa eneo la Busoga. Rais ameniteua kama mmoja ya wale wanaoweza kuchukua jukumu la kukabiliana na umaskini''.

''Mimi si kibaraka kama watu wanavyofikiri, ninajihusisha na mfumo wa kisiasa ambao ndio njia mbadala ya kushirikiana na wakazi wa mashinani na kukabiliana na umaskini,'' ndilo lililokuwa jibu la wakosoaji wake waliosema kuwa amenunuliwa.

Lakini mda mfupi baadaye alikosana na wakazi wa Busoga ,wakiwemo madiwani na maafisa wa kiufundi ambao hawakukubaliana na mbinu zake za kazi.

Wengine walimkosoa na kusema ni mjeuri, lakini alisema kuwa ana lengo la kuafikia ndoto yake ya kuondoa umaskini katika eneo la Busoga, na kwamba hakuna litakalomzuia.

Baadaye Kyalya alikosana na viongozi wa kitamaduni wa Ufalme wa Busoga alipoingilia uongozi wa ufalme huo.

Kwake yeye, isipokuwa Chifu wa Bulamogi Edward Columbus Wambuzi, machifu wengine wote waliosalia walikuwa katika viti hivyo kinyume cha sheria.

Alijitokeza na kuwapanga upya machifu walioteuliwa kwa kufuata sheria katika kila eneo la ufalme na kuapa kuhakikisha kuwa watachukua madaraka, hatua iliyozua mvurugano katika ufalme huo.

Mwaka uliopita baada ya miaka miwili katika afisi, Rais Yoweri Museveni alimwita na kumhakikishia kuwa atampeleka katika wadhifa mwengine, lakini aliondoka na kuelekea nchini Uingereza ambapo amekuwa akiishi hadi hivi majuzi.