Besigye na Muntu waachiliwa huru Uganda

Besigye
Image caption Leo ilikuwa mara ya tatu kwa Besigye kukamatwa wiki hii

Mgombea urais wa chama cha Forum for Democratic Change Dkt Kizza Besigye ameachiliwa huru baada ya kuzuiliwa na polisi kwa saa kadha katika kituo cha polisi cha Nagalama, mke wake Winnie Byanyima amesema.

Dkt Besigye alikamatwa na kuzuiliwa pamoja na rais wa chama cha FDC Jenerali Mugisha Muntu.

Polisi waliwakamata baada ya kuzingira na kuingia ndani kwa nguvu katika afisi kuu za chama hicho ambapo viongozi wakuu wa chama walikuwa wanakutana eneo la Najjanankumbi, Kampala.

Naibu msemaji wa polisi Polly Namaye amenukuliwa na kituo cha televisheni akisema polisi walifika Najjanankumbi baada ya kupokea habari kwamba viongozi wa FDC walikuwa wanajiandaa kujitangazia matokeo.

Bi Byanyima kwa upande wake alisema awali kwamba alizungumza na Besigye ambaye alimwambia anaamini polisi waliwakamata kuwazuia kuhutubia wanahabari.