MOJA KWA MOJA: Yanayojiri Uganda

Bofya hapa kwa habari za karibuni zaidi

23:50 Hapa ndipo tunafikia kikomo cha habari zetu za moja kwa moja kuhusu uchaguzi mkuu Uganda.

Ungana nasi hapo kesho kwa habari zaidi. Shukran na Kwaheri.

22:40 Tume imetangaza matokeo mengine. Kwa sasa katika vituo 14,708 kati ya 28,010, Rais Yoweri Museveni ana kura 3,156,070 (61.27%) naye Kizza Besigye kura 1,767,041 (34.30%).

Matokeo kwa sasa (Vituo 14,708 kati ya 28,010)
Abed Bwanika 51,150 1.00%
Amama Mbabazi 88,900 1.78%
Baryamureeba Venasius 33,135 0.64%
Benon Biraaro 15,588 0.30%
Kizza Besigye 1,767,041 34.30%
Joseph Mabirizi 14,757 0.30%
Maureen Kyalya 24,536 0.50%
Yoweri Museveni 3,156,070 61.37%
Chanzo: Tume ya Uchaguzi Uganda (EC)

22:18 Mgombea urais wa chama cha FDC Dkt Kizza Besigye ameachiliwa huru baada ya kuzuiliwa na polisi kwa saa kadha katika kituo cha polisi cha Nagalama, mke wake Winnie Byanyima amesema.

20:10 Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry amezungumza kwa simu na Rais Yoweri Museveni na kueleza wasiwasi wake kuhusiana na kukamatwa mara kwa mara kwa mgombea urais wa FDC Kizza Besigye.

19:18 Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Badru Kiggundu ametangaza mkumbo mwingine wa matokeo sasa vituo vikifikia 13,305 kati ya jumla ya vituo 28,010. Rais Yoweri Museveni anaongoza akiwa na kura 2,900,109 (62.82%) naye Besigye akiwa na 1,507,495 (32.66%).

Matokeo kwa sasa (Vituo 13,305 kati ya 28,010)
Abed Bwanika 45,370
Amama Mbabazi 80,893
Baryamureeba Venasius 31,331
Benon Biraaro 14,469
Kizza Besigye 1,507,495
Joseph Mabirizi 13,660
Maureen Kyalya 23,076
Yoweri Museveni 2,900,109
Chanzo: Tume ya Uchaguzi Uganda (EC)

18:40 Mke wa Dkt Kizza Besigye, Winnie Byanyima, ameandika kwenye Twitter kwamba kiongozi huyo wa upinzani bado anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nagalama pamoja na Jenerali Muntu. Askari anayewalinda anasema amewapa mkeka wa kulalia.

17:13 Mawaziri kadha katika serikali wameshindwa katika uchaguzi wa ubunge.

Miongozi mwa walioshindwa ni:

 • Waziri wa Ulinzi - Crispus Kiyonga
 • Waziri wa Haki - Kahinda Otafiire
 • Waziri wa Habari - Jim Muhwezi
 • Waziri wa Elimu - Jessica Alupo
 • Mwanasheria Mkuu - Fred Ruhindi

Gazeti la New Vision linasema mawaziri na mawaziri wasaidizi 17 wamepoteza viti vyao vya ubunge.

16:28 Ubalozi wa Marekani mjini Kampala walaani kitendo cha polisi kuvamia makao makuu ya chama cha FDC.

16:22 Maafisa wa usalama wanaendelea kushika doria katika barabara ya Entebbe mjini Kampala. Barabara hiyo imefungwa. Fujo zimezuka katika baadhi ya maeneo ya Kampala.

15:56 Mkuu wa Tume ya uchaguzi Badru Kiggundu amesema matokeo kamili ya uchaguzi yanatarajiwa kufikia saa kumi alasiri kesho. Amesema ni tume pekee yenye idhini ya kutangaza matokeo.

15:44 Maafisa wa usalama wanaendelea kushika doria maeneo mengi Kampala, mwandishi wa BBC Tulanana Bohela anasema.

Image caption Hali ya wasiwasi bado imetanda baadhi ya maeneo ya Kampala

15:25 Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi kuhusu habari za kukamatwa kwa Besigye: "Uganda si sayari nyingine, kuna sheria. Iwapo alikuwa anajaribu kujitangazia matokeo, hebu ajibu kwa makosa yake ya kutofuata sheria."

15:14 Mkuu wa Tume ya uchaguzi Badru Kiggundu ametangaza matokeo ya karibuni zaidi.

Matokeo hayo ni kama ifuatavyo:

Matokeo kwa sasa (Vituo 12,465 kati ya 28,010)
Abed Bwanika 42,270 0.98%
Amama Mbabazi 74,127 1.71%
Baryamureeba Venasius 28,814 0.67%
Benon Biraaro 13,495 0.31%
Kizza Besigye 1,414,708 32.72%
Joseph Mabirizi 12,510 0.29%
Maureen Kyalya 21,663 0.50%
Yoweri Museveni 2,715,914 62.82%
Chanzo: Tume ya Uchaguzi Uganda (EC)

15:06 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Badru Kiggundu ameingia kwenye ukumbi wa Kiprotich, uwanja wa Namboole tayari kutangaza matokeo mengine.

14:09Besigye akamatwa

Kizza Besigye na rais wa FDC Mugisha Muntu wamekamatwa katika makao makuu ya chama hicho Najjanankumbi, kituo cha televisheni cha NBS kimeripoti. Polisi wametumia mabomu ya machozi kutawanya wafuasi wa chama hicho.

13:00 Ripoti zinasema makao makuu ya chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC) yamevamwia na maafisa wa usalama.

12:35 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Badru Kiggundu anatarajiwa kutangaza matokeo mengine mwendo wa saa nane unusu adhuhuri.

11:50 Mitandao ya kijamii nchini Uganda bado imefungwa kwa siku ya pili. Kwa muda mfupi usiku, watu waliweza kuingia mitandao hiyo lakini asubuhi hawakuweza. Jana Rais Museveni alisema hatua hiyo ilichukuliwa kwa sababu za kiusalama.

11:26 Tume ya Uchaguzi imetoa mkumbo wa pili wa matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais ambayo yanaonesha Rais Yoweri Museveni ameweka pengo la kura milioni moja kati yake na Dkt Kizza Besigye.

Matokeo kwa sasa ni kama ifuatavyo:

Matokeo kwa sasa (Vituo 10,246 kati ya 28,010)
Abed Bwanika 35,487
Amama Mbabazi 60,694
Baryamureeba Venasius 23,380
Benon Biraaro 11,176
Kizza Besigye 1,182,025
Joseph Mabirizi 10,266
Maureen Kyalya 18,444
Yoweri Museveni 2,191,283
Chanzo: Tume ya Uchaguzi Uganda (EC)

08:25 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Badru Kiggundu anatarajiwa kutangaza mkumbo wa pili wa matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais.

Matokeo ya mkumbo wa kwanza kutoka kwa tume hiyo ya uchaguzi yanaonesha Rais Museveni anaongoza akifuatwa na Dkt Kizza Besigye. Matokeo ni kutoka vituo 6,448 kati ya 28,010

 • Abed Bwanika 22,180 (1.0%)
 • Amama Mbabazi 41,291 (1.87%)
 • Baryamureeba Venasius 15,260 (0.69%)
 • Benon Buta Biraaro 7,228 (0.33%)
 • Kizza Besigye 738,628 (33.47)
 • Mabirizi Joseph 6,833 (0.31%)
 • Maureen Kyalya 12,742 (0.58%)
 • Yoweri Museveni 1,362,961 (61.75%)

07:05 Mgombea urais wa chama cha FDC Dkt Kizza Besigye yuko huru baada ya kukamatwa na kuzuiliwa kwa muda na maafisa wa polisi jana.

Besigye pamoja na meya wa zamani wa Kampala Elias Lukwago walifika katika kile polisi wanasema ni jumba lao eneo la Naguru, Kampala na kutaka kuingia ndani kufanya ukaguzi. Dkt Besigye na wenzake walidai kilitumiwa kuiba kura. Polisi wamekanusha hayo.

Msemaji wa polisi wa Kampala Patrick Onyango amesema ni mkuu wa polisi pekee anayeweza kutoa idhini kwa mtu kuingia ndani.

“Dkt Kizza Besigye alikamatwa kwa kujaribu kuingia eneo lisiloruhusiwa na baadaye aliachiliwa kwa bondi ya polisi. Alipelekwa nyumbani kwake Kasangati. Uchunguzi zaidi kuhusu kisa hiki unaendelea,” alisema kupitia taarifa.

Image caption Besigye akiwa hoteli ya Imperial Royale, Kampala baada ya kuachiliwa huru

07:50 Hujambo! Twatumai umeamka salama na buheri wa afya. Karibu kwa taarifa za moja kwa moja kuhusu yanayojiri nchini Uganda baada ya uchaguzi mkuu kufanyika hapo jana.

Kura zinaendelea kuhesabiwa katika maeneo mengi. Katika baadhi ya vituo mjini Kampala na wilaya ya Wakiso ambapo uchaguzi ulitatizika, upigaji kura utaendelea leo.