Marekani yashambulia kambi ya IS Libya

Image caption Ramani ya Libya

Maafisa wa Marekani wamethibitisha kuwa ni ndege za Marekani zilizofanya mashambulio huko Libya wakiwalenga wanamgambo wa IS.

Hata hivyo shambulio hilo la karibu na mji wa Sabratha,lililonuiwa kumlenga hasa mpiganaji mmoja wa Tunisia limeripotiwa kuwauwa watu 30 .

Mpiganaji huyo wa Tunisia anasemekana ndiye aliyefanya shambulio la mwaka jana katika kumbukumbu za Bardo na hoteli ya ufuoni mwa bahari ya Sousse huko Tunisia ambako watu zaidi ya 10 waliuawa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mshambulizi ya ndege za Marekani

Mashambulio hayo yalilenga kambi moja ya wapiganaji wa Islamic State na kumuua kiongozi mmoja mwenye itikadi kali ,maafisa wa Marekani wamesema.

Noureddine Chouchane anahusishwa na mashambulio mawili nchini Tunisia mwaka uliopita ,ikiwemo shambulio lililowaua raia 30 wa Uingereza.

Kundi la IS limekuwa likifanya oparesheni zake nchini Libya kwa kipindi cha mwaka mmoja na Marekani inakadiria kwamba lina hadi wapiganaji 6,000 nchini humo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wapiganaji wa Islamic State

Libya inasalia katika machafuko ya wenyewe kwa wenyewe miaka minne baada ya kupinduliwa kwa aliyekuwa kiongozi wake Muammar Gaddafi,na inapiganiwa na makundi tofauti ikiwemo kundi la IS.