Magufuli apiga marufuku uingizaji wa sukari

Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania

Rais John Magufuli wa Tanzania amepiga marufuku uingizaji wa sukari kutoka mataifa ya kigeni ili kuvilinda viwanda vya sukari nchini humo ambavyo vimeathiriwa na uingizaji wa sukari ya bei rahisi kutoka nje.

Rais huyo amesema kuwa taifa hilo haliwezi kuafikia malengo yake ya kuimarika kwa viwanda vyake iwapo viwanda vya sukari nchini humo havitalindwa na kuwezeshwa dhidi ya uingizaji huo.

''Tuna viwanda nchini ambavyo hununua miwa kutoka kwa wakulima wadogo wadogo.Viwanda hivi huzalisha sukari,ajira na ni chanzo cha mapato ya serikali.Ijapokuwa tuna hifadhi ya kutosha ya sukari ,kuna watu serikalini wanaotoa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje ,''alisema akiwa katika ikulu ya Dar es Salaam.

''Hawa watu wanakandamiza juhudi za serikali...hivyobasi natangaza kwamba hakuna vibali vitakavyotolewa kuruhusu uingizaji wa sukari,hadi iwapo kutakuwa na mahitaji maalum,''aliongezea.

Image caption sukari

Amesema baadhi ya sukari hiyo inayoingizwa nchini imeisha mda wake na haifai kutumiwa na binaadamu.

Mahitaji ya bidhaa hiyo muhimu nchini Tanzania ni tani 420,000 huku tani 170,000 zikitumika kwa mahitaji ya nyumabni na sukrai ya viwandani na hivyobasi kuwa tani 590,000 kila mwaka.

Huku viwanda vya Tanzania vikizalisha tani 300,000, kila mwaka kuna upungufu wa tani 290,000 za matumizi ya nyumbani na yale ya viwandani.