Papa Francis alegeza msimamo kuhusu Zika

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Papa Francis azungumza kuhusu virusi vya Zika

Papa Francis amesema kuwa utumizi wa vifaa vya kupanga uzazi miongoni mwa wanawake walio katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Zika unaweza kukubalika.

Papa Francis amesisitiza kuwa uavyaji mimba ni uhalifu lakini kuzuia mimba si uovu wa moja kwa moja.

Matamshi yake yanajiri kujibu swali la kukabiliana na mlipuko wa Zika katika mataifa ya Marekani Kusini.

Virusi hivyo vinahusishwa na kasoro ya watoto wanaozaliwa na vichwa vidogo ambayo huathiri ukuaji wa mtoto.

Image caption Mtoto aliyeathirika na virusi vya Zika

Kanisa katoliki linapiga marufuku utumizi wa vifaa vya kuzuia mimba.

''Hatufai kufananisha uovu wa kuzuia mimba na ule wa kutoa mimba ,''Papa francis aliwaambia wanahabari katika ndege alipokuwa akirudi kutoka ziara ya Mexico.