Aliyefungwa jela miaka 43 Marekani aachiliwa huru

Woodfox Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Woodfox alidaiwa kumuua askari jela mwaka 1972

Mwanamume aliyefungwa kifungo cha upweke jela muda mrefu zaidi katika historia ya Marekani ameachiliwa huru baada ya kuwa gerezani miaka 43.

Albert Woodfox, amekuwa akizuiliwa katika jimbo la Louisiana.

Mawakili wake wanasema alikuwa akizuiliwa kwenye seli saa 23 kila siku.

Woodfox ndiye pekee aliyesalia gerezani kutoka kwa kundi la wafungwa lililojulikana kama "Angola Three" (Watatu wa Angola), ambao walikaa sana jela.

Jina Angola linatokana na shamba kubwa lililo karibu na gereza hilo.

Amekuwa akitumikia kifungo cha upweke tangu Aprili 1972 baada ya kudaiwa kumuua askari jela.

Alikanusha shtaka la kumuua askari huyo Brent Miller.

Wakati wa kuuawa kwa Brent, Woodfox alikuwa amefungwa jela kwa wizi wa mabavu na uvamizi

Haki miliki ya picha
Image caption Wakati wa kuuawa kwa Brent, Woodfox alikuwa amefungwa jela kwa wizi wa mabavu na uvamizi

Woodfox, 69, mwishowe ameachiliwa baada ya kukiri shtaka lenye adhabu nafuu kidogo la kuua bila kukusudia.

Inadaiwa waendeshaji mashtaka wa serikali wamehusika kumshawishi akubali akosa hilo ndogo.

Ingawa amekubali kosa hilo, anasema si ishara kwamba alikuwa na hatia.

“Ingawa nilisubiri kuthibitisha kwamba sikuwa na makosa, wasiwasi kuhusu afya yangu na uzee pia vimenifanya kuamua kufikisha kikomo cha mambo haya yote na kupata uhuru wangu kwa kukiri shtaka la lenye adhabu ndogo,” alisema kupitia taarifa Ijumaa.

Haki miliki ya picha AP

Kabla ya kuondoka gereza lililoko eneo la Feliciana, St Francisville, akiandamana na kakake, Woodfox ameambia wanahabari kwamba alitaka kwanza kutembelea kaburi la mamake.

Mamake huyo alifariki akiwa gerezani na Woodfox hakuruhusiwa kuhudhuria mazishi.