Touadera ashinda urais Afrika ya Kati

Touadera Haki miliki ya picha AFP
Image caption Touadera ameahidi kuimarisha usalama

Waziri mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin Touadera ameshinda duru ya pili ya uchaguzi nchini humo.

Matokeo ya awali yanaonesha Bw Touadera alipata karibu 63% ya kura zilizopigwa, na kumshinda mpinzani wake Anicet Dologuele 37% kwenye uchaguzi huo uliofanyika tarehe 12 Februari.

Kwenye kampeni yake Bw Touadera aliangazia sana kurejesha usalama.

Taifa hilo limekubwa na mapigano ya kidini kwa miaka kadha.

Vita vilianza 2013 baada ya waasi wa Kiislamu wa Seleka kuchukua mamlaka.

Bw Touadera, kwenye kampeni yake, alioneshwa na wafuasi wake kama mpenda amani ambaye angeweza kupatanisha Waislamu na Wakristo na kufufua uchumi.

Haki miliki ya picha
Image caption Bw Dologuele ameahidi kukubali matokeo

Akihutubia wanahabari Jumamosi usiku, Bw Dologuele alisema atakubali matokeo ingawa alisema kulikuwa na kasoro za hapa na pale.

Bw Touadera ameahidi kufanikisha maridhiano na kuhakikisha raia wanasalimisha silaha.

"Uchaguzi huu ni muhimu lakini sio hatua pekee ya kututoa kutoka kwa mgogoro huu. Lazima tuweke mazingira ya kufanikisha mazungumzo kati ya pande zote mbili. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaishi pamoja kwa amani.”

Bw Touadera alikuwa profesa katika hesabu na alihudumu kama waziri mkuu chini ya utawala wa Francois Bozize.

Bw Bozize aliongoza miaka 10 hadi serikali yake ilipopinduliwa mwaka 2013 na akatorokea uhamishoni.