Ethiopia yakana kuwadhulumu watu wa Oromo

Maandamano ya watu wa jamii ya Oromo

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Maandamano ya watu wa jamii ya Oromo

Ripoti mpya imeshutumu vikosi vya usalama nchini Ethiopia kwa kutekeleza zaidi ya miezi minne ya mauaji, ukatili na kukamatwa kwa mamia ya waandamanaji katika eneo la Oromia.

Shirika la Human Rights Watch linasema vikosi hivyo, vimetumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano hayo yaliyoanza Novemba 2015, kupinga mipango ya kupanua mamlaka ya jiji kuu la Addis Ababa.

Serikali imekanusha ripoti hiyo.

HRW inasema kuwa vikosi vya usalama ikiwemo jeshi, inadaiwa kufanya misako mikali dhidi ya waandamanaji katika eneo la Oromia.

Oromia ndilo jimbo kubwa zaidi nchini Ethiopia.

Maandamano hayo yalianza kufuatia tangazo la kuipanua jiji kuu la Addis Ababa.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Vikosi vya usalama nchini Ethiopia vinadaiwa kutekeleza zaidi ya miezi minne ya mauaji, ukatili na kukamatwa kwa mamia ya waandamanaji wa Oromo

Kutekelezwa kwa mpango huo wapinzani wanasema, lingewaondoa wakulima wa Oromia kutoka mashamba yao.

Serikali hata hivyo tayari imefutilia mbali mpango huo.

Hata hivyo makabiliano kati ya waandamanaji na polisi yameendelea kutokea mwaka huu.

Waliohojiwa na HRW wamesimulia jinsi polisi walivyotumia vitoa machozi na risasi kuwatawanya waandamanaji, huku maelfu ya wengine wao wakikamatwa.

Waandamanaji wengine walikuwa na umri wa miaka kumi pekee.

Chanzo cha picha,

Maelezo ya picha,

Mamia ya waandamanaji katika eneo la Oromia hawajulikani waliko

Wale waliokamatwa ni pamoja na wanafunzi, wanahabari, na viongozi wa upinzani wanaounga mkono Oromo.

Waziri wa masuala ya serikali Getachew Reda amekanusha madai yaliyomo katika ripoti hiyo.

Ameiambia BBC kuwa serikali inafanya uchunguzi wake wa kibinafsi kubaini idadi ya watu waliokamatwa au kufariki katika makabiliano hayo.

Hadi kufikia sasa idadi kamili ya watu waliofariki tangu makabiliano hayo kuanza miezi minne iliyopita, haijabainika.