Gari la dereva wa Uber lachomwa moto Kenya

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Dereva wa Uber achomwa moto Kenya

Mzozo kati ya kampuni ya taxi ya Uber na madereva na teksi za kibinafsi, umechukua mkondo mpya baada ya dereva mmoja wa Uber kushambuliwa na gari lake kuteketezwa mjini Nairobi.

Pande hizo mbili zimekuwa zikilumbana tangu Uber ilipoanza kutoa huduma zake mjini Nairobi.

Dereva mmoja wa teksi wa kampuni maarufu yenye makao yake nchini Marekani Uber, anauguza majeraha katika hospitali moja mjini Nairobi, baada ya kushambuliwa na watu wanaoaminika kuwa madera za taxi za kawaidi nchini Kenya.

Akithibitisha tukio afisa mkuu wa polisi Japheth Koome, amesema kuwa dereva huyo alivamiwa na genge hilo kabla ya gari lake kuteketezwa wakati wa tukio hilo lililotokea jana usiku.

Koome amesema kuwa uchunguzi umeanzishwa na tayari wamepata vidokezo kutoka kwa kanda za video kutoka eneo hilo la tukio, na kuwa maafisa wa polisi kwa sasa wanawasaka washukiwa hao pamoja na gari lililotumika kufanya shambulio hilo.

Meneja wa kampuni hiyo katika kanda ya mashariki na kusini mwa Afrika, Alon Lits, amesema amehuzunishwa na tukio hilo na kuwa wamezungumza na dereva aliyejeruhiwa na kuwa yuko katika hali nzuri.

Image caption Kumekuwa na malumbano nchini Kenya kati ya kampuni hiyo ya Uber na teksi za kawaida

Lits ameongeza kusema kuwa tayari wamewasilisha malalamiko yao kwa serikali, ili kuhakikisha waliohusika wamefikishwa mahakamani.

Kumekuwa na malumbano nchini Kenya kati ya kampuni hiyo ya Uber na teksi za kawaida, huku wamiliki wa teksi za kawaida wakilalamika kuwa kampuni hiyo, ilikuwa inahujumu biashara yao kwa kulipisha ada ndogo.

Aidha kampuni hiyo ya Uber imetuhumiwa kutolipa ada nyinginezo kama gharama ya maeneo ya kupakia magari, ada ya baraza la mji na leseni ya kubeba abiria madai ambayo kampuni hiyo ya Uber imeyakanusha.

Mazungumzo ya kutatua mzozo huo wa taxi nchini Kenya, yameanza chini ya usimamizi wa wizara ya uchukuzi, lakini kufikia sasa hakuna maafikiano yoyote, hali ambayo imefanya uhasama kati ya makundi hayo mawili kutokota.

Shambulio hilo la jana ndilo la kwanza dhidi ya kampuni hiyo ya Uber, na polisi nchini Kenya wanasema hawataruhusu madereva hao wa kibinafsi kuwatishia wenzao wa Uber