Bei ya mafuta: Buhari kushirikiana na Saudia

Image caption Buhari kushirikiana na Saudia

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameahidi kushirikiana na Saudi Arabia kuhakikisha bei ya mafuta inapanda.

Rais Buhari ambaye yuko mjini Riyadh ameahidi kushirikiana na mfalme Salman kuhakikisha bei ya bidhaa hiyo muhimu inaimarika.

Bei ya mafuta ilishuka kwa hadi chini ya dola 30 baada ya mataifa yanayozalisha dhahabu hiyo nyeusi kushindwa kukubaliana kupunguza bidhaa hiyo sokoni.

Msemaji wa wa rais Buhari Garba Shehu anasema kuwa kiongozi huyo wa taifa tajiri zaidi barani Afrika yuko mbioni kuhakikisha kuwa kitega uchumi chao kinanunuliwa kwa bei stahiki.

Mataifa yote mawili yanategemea kwa asilimia kubwa mapato kutokna na mauzo ya mafuta.

Kuporomoka kwa bei ya mafuta kutoka dola mia moja kwa pipa hadi dola 30 kumeathiri sana chumi za Saudia na Nigeria.

Serikali zote mbili zimelazimika kukata huduma muhimu kutokana na nakisi kubwa ya bajeti.

Hatua hiyo imesababisha mfumuko wa bei ya bidhaa muhimu kama chakula huduma za afya na kawi.

Gazeti moja la saudia limechapisha picha ya rais Buhari akikagua gwaride la heshma akiwa na mwenyeji wake mfalme Salman.