Johnson & Johnson kulipa fidia ya $72m

Poda ya Johnson Haki miliki ya picha Getty
Image caption Poda ya Johnson inasemekana kuwa chanzo cha saratani ya ovari iliyomuua Jackie Fox

Jopo la mahakama katika jimbo la Missouri limeiamrisha kampuni ya Johnson & Johnson (J&J) kulipa dola milioni 72 kwa familia ya mwanamke aliedai kifo chake kilikua na uhusiano na matumizi ya poda ya watoto ya talc, inayotengenezwa na kampuni ya Johnson&Johnson.

Jackie Fox kutoka Birmingham, Alabama alifariki kwa maradhi ya saratani ya Ovari mwaka jana, akiwa na umri wa miaka 62, baada ya kutumia poda ya talc kwa miongo kadhaa. Familia yake ilidai kwamba kampuni hiyo ilifahamu fika hatari za talc lakini haikuwaonya watumiaji.

Haki miliki ya picha SPL
Image caption familia ya Jacky Fox inasema alipata satarani ya Ovari baada ya kutumia poda ya Johnson&Johnson

J&J ilikanusha madai hayo na kusema kuwa inaangalia uwezekano wa kukata rufaa. Watafiti wanasema uhusiano kati ya matumizi ya poda hiyo na saratani ya Ovari haujathibitishwa . Masemaji wa kampuni hiyo amesema: "Hatuna wajibu mkubwa kuliko afya na usalama wa wanunuzi wetu, na tunasikitishwa na matokeo ya kesi.

"tunaionea huruma familia ya mlalamikaji , lakini tunaamini kabisa usalama wa kipodozi talc umekua ukifuatiliwa kwa miongo kadhaa na ushahidi wa kisayansi upo."

Uamuzi huo uliotolewa baada ya kesi iliyochukua wiki tatu ni wa kwanza ambapo jopo la Mahakama ya Marekani limeamuru kulipwa kwa gharama kwa madai kuhusiana na poda ya talc. Zaidi ya visa 1000 vya aina hiyo viko kote nchini Marekani na mawakili wanasema maelfu zaidi ya watu wanaweza kuwasilisha kesi zao Mahakamani.