Ebola ina madhara ya kudumu kwa afya

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ebola ina madhara ya kudumu kwa afya

Utafiti umebaini kuwa wahasiriwa wa ugonjwa wa Ebola wana madhara mengi tu ya kiafya hata baada ya kusemekana kuwa wamepona maambukizi hayo.

Madaktari katika taasisi ya afya nchini Marekani (US National Institutes of Health) wamegundua kuwa idadi kubwa ya wahathirika wa Ebola wamepatikana kuwa na upungufu mkubwa wa kinga mwilini, kupoteza kumbukumbu mbali na kukumbwa na msongo wa mawazo takriban miezi 6 tangu waondoke katika vituo vya matibabu ya wagonjwa wa Ebola.

Wengi wa waathiriwa wa ugonjwa huo wa Ebola wametishia kujitia kitanzi.

Zaidi ya watu 17,000 Magharibi mwa Afrika walipona kufuatia maambukizi ya Ebola.

Utafiti huo ulitolewa katika kongamano la madaktari wa maradhi ya kiakili (Academy of Neurology), kama sehemu ya mwanzo mwanzo wa utafiti wa kina kuhusu madhara ya Ebola.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maambukizi ya Ebola huathiri vibaya uwezo wa mwili kupambana na maradhi mengine.

Uchunguzi wa awali wa waathiriwa 82, ulithibitisha kuwepo kwa matatizo ya kisaikolojia na maradhi ya kiakili kama vile homa kali ya uti wa mgongo na hata kukosa ufahamu kabisa wakati maradhi hayo hayajadhibitiwa.

Thuluthi mbili ya wahasiriwa iliripoti udhaifu wa mwili, mauamivi ya kichwa ya mara kwa mara,msongo wa mawazo, ndoto za kutisha na wakati mwengine usahalifu.

Wawili kati yao walijaribu kujiua wakati wa utafiti huu.

Daktari Lauren Bowen, kutoka kwa taasisi ya magonjwa ya kiakili ameiambia BBC kuwa ''inasikitisha kuwa vijana hao wachanga wanakabiliwa na magonjwa ambayo kwa kawaida yanahusishwa na watu wenye umri mkubwa''.

''kwa vijana wanaokwenda shuleni bila shaka wanasusia kurejelea masomo yao na kama ni waajiriwa hata kazi huwashinda na wengi wanashindwa kupata usingizi.

''Kwa vijana hao Ebola haijawaondokea maishani mwao.''

Maambukizi ya Ebola huathiri vibaya uwezo wa mwili kupambana na maradhi mengine.

Dalili zingine hupotea mara moja lakini zingine huchukua muda mrefu kufifia.

Image caption Mara nyingi tumewapata wakiwa na maradhi ya macho.

Vile vile utafiti umegundua kuwa asilimia 38% ya wanaume wamepatikana wakiwa na virusi vya Ebola katika mbegu zao za kiume takriban mwaka mmoja baada ya kupona Ebola.

Katika kisa kimoja mwanaume mmoja alipatikana na virusi vya Ebola takriban mwaka mmoja u nusu baadaye.

Hali hiyo imesababisha taharuki ya kurejea kwa mlipuko wa Ebola kwani wanaume 4 kati ya 100 ndio wanaoujikinga wakati wanaposhiriki mapenzi kwa kutumia mpira.

Kimsingi madaktari hao wanasema kuwa itachukua muda mrefu kuelewa madhara ya Ebola kwa afya wa waathirika waliopona.