Daktari mkeketaji apokonywa leseni Misri

Image caption Suhair al Bataa

Mahakama nchini Misri hatimaye imempokonya leseni daktari aliyepatikana na hatia ya mauaji ya kutokusudia ya msichana wa miaka 13 ambaye alifariki baada ya kufanyiwa ukeketaji.

Raslan Fadl alikuwa daktari wa kwanza nchini Misri kuwahi kushtakiwa na ukeketaji,hata baada ya uovu huo kupigwa marufuku 2008.

Hukumu yake ya miaka 2 jela ilipongezwa kuwa ushindi mkubwa na wanaharakati wanaokabiliana na ukeketaji.

Lakini ripoti za hivi karibuni zilisema kuwa Fadl hakufungwa na kwamba bado alikuwa anaendelea kuhudumu kama daktari.

Licha ya marufuku hiyo ,zaidi ya wasichana asilimia 90 na wanawake walio na umri wa kati ya miaka 15 na 59 nchini humo wamekeketwa katika miaka ya hivi karibuni ,kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.