Raia wapiga kura kuwachagua viongozi Iran

Bunge Haki miliki ya picha ISNA
Image caption Uchaguzi huo ni wa wabunge na wawakilishi wa kidini

Mamilioni ya raia wa Iran wanapiga kura kuwachagua wabunge, kwenye uchaguzi wa kwanza tangu kutiwa saini kwa mkataba uliopelekea kuondolewa kwa vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya taifa hilo.

Wapiga kura pia wanawachagua wawakilishi wao katika Baraza la Wataalamu, ambalo ni kundi la kidini linalomteua Kiongozi Mkuu.

Wanaounga mkono mageuzi wanatumai kwamba wataongeza ushawishi wao katika taasisi hizo mbili, zilizodhibitiwa na wahafidhina.

Matokeo ya uchaguzi huo huenda yakaathiri uwezekano wa Rais Hassan Rouhani kuchaguliwa tena 2017.

Kiongozi Mkuu wa kidini Ayatollah Ali Khamenei ametoa wito kwa wapiga kura kujitokeza kwa wingi “kuaibisha maadui wa Iran”.

“Yayote anayeipenda Iran na hadhi yake, ukuu wake na fahari yake anafaa kupiga kura. Iran ina maadui. Na wanatuangalia kwa tamaa…Watu wanafaa kuwa macho na kupiga kura kwa makini na busara,” amesema baada ya kupiga kura.

Wapiga kura wanawachagua wabunge 290, watakaohudhumu kwa muhula wa miaka minne pamoja na wawakilishi wa kidini 88 wa kuhudumu katika Baraza la Wataalamu kwa muhula wa miaka minane.

Wataochaguliwa kuhudumu katika Baraza la Wataalamu huenda wakapata fursa ya kuchagua mrithi wa Ayatollah Khamenei, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 76 na anatatizwa na afya.