Mkataba wa kusitisha vita Syria wavunjwa

Haki miliki ya picha epa
Image caption Watoto walipata fursa ya kucheza nje baada ya mkataba wa kusitisha mapigano kutekelezwa

Ndege za jeshi zimeshambulia maeneo kadha ya kaskazini mwa Syria, siku moja baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa nchini humo.

Wanaharakati wa huko wanafikiri mashambulio hayo yamefanywa na Urusi, ambayo inasaidia majeshi ya Rais Bashar al-Assad kukabiliana na waasi.

Upinzani umelalamika kuwa makubaliano yamevunjwa mara 15 na upande wa serikali.

Warusi pia wanasema, wameona visa kadha kinyume na mkataba, lakini kwa jumla, usitishwaji wa mapigano unaendelea.

Awali Mawaziri wa mashauri ya Kigeni wa Marekani na Urusi, John Kerry na Sergei Lavrov, wamekaribisha mwanzo wa usitishaji mapigano nchini Syria.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanaharakati wa huko wanafikiri mashambulio hayo yamefanywa na Urusi, ambayo inasaidia majeshi ya Rais Bashar al-Assad

Ingawa kumekuwa na ripoti za wapiganaji kukiuka mapatano hayo ya usitishaji mapigano lakini kwa ujuma hali imetulia.

Maeneo yaliyokuwa na mapigano makali ya Aleppo yametajwa kuwa tulivu.

Bwana Kerry na Bwana Lavrov walizungumzia uwezekano wa kuanzisha mashauriano ya amani, ambayo Umoja wa Mataifa unatarajia yataanza juma lijalo.

Wapiganaji wa Islamic State ambao hawashirikishwi katika usitishaji huo wa mapigano, walifanya mashambulizi dhidi ya mji wa Tal Abyad, Kaskazini mwa Syria.

Wapiganaji Wakurdi walisema kuwa mashambulizi hayo yalizimwa.