Al-Shabab: Kenya yaimarisha doria viwanja vya ndege

al-shabab
Image caption Wanamgambo wa al-Shabab wamekuwa wakitekeleza mashambulio mara kwa mara Kenya

Kenya imeimarisha usalama katika viwanja vikuu vya ndege baada ya habari za kijasusi kudokeza huenda wanamgambo wa al-Shabab kutoka Somalia wakawa wanapanga mashambulio.

Waraka wa siri kutoka afisa mkuu wa usalama wa viwanja vya ndege Bw Eric Kiraithe unasema kuna washambuliaji 11 wa kujitoa mhanga ambao wamepokea mafunzo na kutumwa Kenya.

“Washambuliaji watano watashambulia uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na hao wengine kuangazia viwanja vya ndege Pwani, na sana uwanja wa kimataifa wa Moi,” waraka huo unasema.

Maafisa wa usalama wamekiri kwamba waraka huo ulitumwa lakini wakasema habari hizo zilifaa kuwa siri na kwamba walikuwa wanachukua tahadhari.

Hata hivyo wamekiri kuwa wameimarisha usalama ingawa wanasema si kutokana na habari za kijasusi kwamba huenda viwanja vya ndege vikashambuliwa.

Meneja mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA) Yatich Kangungo amesema uchunguzi unaendelea kubaini nani aliyefichua waraka huo na kwamba atachukuliwa hatua za kinidhamu.

"Kwa maafisa hao, waliokiuka itifaki, kuna mfumo wa kuwaadhibu. Kwa sasa tuna habari kuwahusu, na tuna uhakika karibu asilimia mia kwamba habari hizi zilifichuliwa na mmoja wa maafisa wetu walioko Wajir.”

Bw Kiraithe ameambia wanahabari kwamba kawaida huwa wanachukua hatua kila wanapopata habari, hata kama hazijahibitishwa.

“Kwa sasa, hakuna thibitisho lolote kwamba viwanja vyetu vya ndege vimo hatarini. Lakini hatuwezi kufumbia macho hali ya sasa ya hatari ya ugaidi duniani.”

Hayo yamejiri wakati ambapo Inspekta mkuu wa polisi Joseph Boinet amethibitisha kwamba al-Shabab bado wanapanga kutekeleza mashambulio Kenya, na hasa maeneo ya kaskazini na pwani ya Kenya pamoja na miji.