Mumtaz Qadri anyongwa

Qadri Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mumtaz Qadri

Maafisa nchini Pakistan wamesema aliyekuwa mlinzi wa gavana wa jimbo la Punjab ambaye alimuua bosi wake kwa risasi, amenyongwa.

Mumtaz Qadri alimuua Salman Taseer mjini Islamabad mwaka 2011, kutokana na upinzani wake dhidi ya sheria za kumkufuru mungu, mauaji ambayo yaliitikisa nchi.

Qadri aliitwa shujaa na baadhi ya makundi ya kiislamu yenye msimamo mkali na maelfu ya wanaharakati wenye msimamo mkali waliandamana kuonesha kumuunga mkono wakati huo.

Baada ya taarifa hizo za kuhukumiwa kunyongwa kundi la watu liliingia tena mtaani kupinga.

Shirika la Habari la AFP limeripoti kuwa vyombo vya ulinzi vimewekwa katika hali ya tahadhari, ikiwemo polisi wa kutuliza ghasia katika maeneo yaliyozunguuka makaazi ya Qadri mjini Islamabad.

Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika kesho karibu na mji wa Rawalpindi, ambako idadi kubwa ya waombolezaji inatarajiwa kushiriki.

Maafisa wa magereza nchini humo wamesema Qadri alinyongwa katika gereza la Adiala mjini Rawalpindi karibu na mji mkuu, Islamabad.