Osama aliacha dola milioni 29 kufadhili Jihad

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Osama aliacha dola milioni 29 kufadhili Jihad

Kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda Osama Bin Laden aliacha urathi wa dola milioni 29 kufadhili Jihad alipouawa mwaka 2011.

Hayo ni kwa mujibu wa wasia wake uliofichuliwa leo na maafisa wa Marekani kwa vyombo vya habari nchini humo.

Aliihimiza familia yake kuheshimu wasia wake na kuwashauri ''watumie mali yake yote kuendeleza jihad''.

Mali yake na wasia wake ni miongoni mwa maelfu ya stakabadhi muhimu zilizofichuliwa hii leo na maafisa wa Marekani.

Aidha Bin Laden alimtaka babake amtunzie mke na wanawe endapo ataaga dunia.

Kiongozi huyo wa al-Qaeda aliuawa na majeshi ya Marekani mwaka wa 2011 katika shambulizi la kufumania lililotekelezwa nchini Pakistan.