Kesi ya kupinga ushindi wa Museveni kuanza

Mbabazi Haki miliki ya picha
Image caption Bw Mbabazi alimaliza wa tatu kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na tume

Kesi ya kupinga ushindi wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi uliopita itaanza kusikizwa Jumatatu.

Uamuzi huo umetolewa baada ya kufanyika kwa kikao cha maandalizi ya kesi ambacho kwa mara ya kwanza kimewakutanisha majaji na mawakili wa pande zote.

Kesi hiyo iliyowasilishwa na waziri mkuu wa zamani Bw Amama Mbabazi katika Mahakama ya Juu nchini humo inahusisha mawakili zaidi ya 100.

Kwenye kikao cha leo kilichofanyika majengo ya mahakama katika mtaa wa Kololo, Kampala majaji wamekubali mabadiliko yaliyofanyiwa kwenye nyaraka za kesi na mawakili wa Bw Mbabazi.

Mbabazi, aliyeibuka wa tatu kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi, anasema uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.

Anataka kura zihesabiwe tena katika wilaya 45, Kampala na Wakiso zikiwa miongoni mwa wizara hizo.

Kwenye nyaraka zao za kesi, mawakili wa Bw Mbabazi wanasema wakati wa kutangazwa kwa matokeo kulikuwa na kura 1.8 milioni ambazo hazikuwa zimehesabiwa.

Aidha, wanadai Rais Museveni aliwahonga wapiga kura eneo la Busoga kwa kuwapa ardhi ya hekta 500. Wanasema alikabidhi ardhi hiyo iliyokuwa sehemu ya hifadhi ya msitu wa Bukaleeba kwa familia 30,000 wakati wa kampeni „kwa lengo la kuwashawishi kumpigia kura uchaguzi wa 2016”.

Image caption Bw Besigye amekuwa kwenye kizuizi cha nyumbani

Mgombea wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC) Dkt Kizza Besigye, aliyemaliza wa pili, hakufanikiwa kuwasilisha kesi ya kupinga uchaguzi wa Rais Museveni katika muda ulioruhusiwa ingawa alikuwa ametangaza kwamba hakukubali matokeo hayo.

Kesi hiyo ya Bw Mbabazi inasikizwa na majaji tisa ambao wana muda wa siku 30 kuisikiza na kutoa uamuzi.

Uamuzi unatarajiwa kutolewa kufikia tarehe 1 Aprili.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na tume, Bw Museveni alipata asilimia 60.7 ya kura, Dkt Besigye asilimia 35.4 na Bw Mbabazi asilimia 1.39.