Aliyeiba dola milioni 20 Nigeria rumande

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kamanda mkuu wa Jeshi aliyeiba dola milioni 20 Nigeria afungwa rumande

Mahakama moja nchini Nigeria imemnyima dhamana aliyekuwa mkuu wa jeshi nchini humo .

Aliyekuwa Mkuu wa jeshi la wanahewa amiri jeshi huyo wa jeshi la angani , Alex Badeh anakabiliwa na mashtaka kumi ya ufisadi ukiukaji wa maadili ya maafisa wa umma mbali na ubadhirifu wa mali ya umma miongoni mwa mashtaka mengine.

Afisa huyo wa ngazi ya juu jeshini anatuhumia kwa kuiba dola milioni 20 kutoka kwa jeshi la wanahewa la Nigeria.

Alex Badeh anasemekana kutumia fedha hizo kununua nyumba ya kifahari mjini Abuja na mali nyingine nchini humo.

Aidha mahakama hiyo ilifahamishwa kuwa maafisa wa polisi walinasa zaidi ya dola milioni moja pesa taslim nyumbani kwake.

Badeh, aliteuliwa mkuu wa majeshi nchini Nigeria miaka miwili iliyopita wakati jeshi la nchi hiyo lilipo shutumiwa kwa kushindwa kukabiliana na wapiganaji wa kiislamu wa Boko Haram.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Badeh, aliteuliwa mkuu wa majeshi nchini Nigeria miaka miwili iliyopita wakati jeshi la nchi hiyo lilipo shutumiwa kwa kushindwa kukabiliana na wapiganaji wa kiislamu wa Boko Haram.

Afisa huyo sasa anajumuika na maafisa wengine wa ngazi ya juu katika serikali ya zamani ya Nigeria wanaotuhumiwa kuiba mabilioni ya dola kutoka kwa hazina na idara ya jeshi.

Katika enzi ya rais wa zamani Goodluck Jonathan, wanajeshi wa Nigeria waliokuwa wakipambana na wapiganaji wa Boko Haram, walilalamika kuwa hawakua na vifaa vya kutosha na vya kisasa kukabiliana na wapiganaji hao wa kiislamu ambao wanasemekana kuwa walikuwa wamejihami kwa vifaa nzito nzito vya kijeshi.

Tangu wakati huo nidhamu katika jeshi la nchi hiyo ilishuka huku wanajeshi wakikataa kutekeleza maagizo waliopewa na wakubwa wao.