Ukimwi: Mbeki atuhumiwa kupotosha umma

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ukimwi: Mbeki anapotosha uma

Magazeti na vyombo vya habari kwa jumla nchini Afrika Kusini leo vimekuwa vikijadili sera ya ukimwi ya rais wa zamani wa nchi hiyo Thabo Mbeki.

Swala hilo limeibuka upya baada ya Mbeki kujaribu kujieleza kupitia kwa blogu yake kuwa hakuwahi kukataa kuwa virusi vya HIV ndivyo vinavyosababisha Ukimwi.

''Sijawahi kudai kuwa virusi vya HIV ndivyo vinavyosababisha ukimwi ''

Wakati wa utawala wake Mbeki alituhumiwa kwa kukanusha madhara yanayoletwa na maambukizi ya HIV/Ukimwi.

''Ukosefu wa kinga mwilini unaletwa na mseto wa maradhi ambayo chanzo chake kinafahamika. Ukosefu huo hauwezi kusababishwa na kirusi hicho kimoja '' Alihoji bwana Mbeki.

''Kulingana nami (Mbeki) Ukosefu wa kinga kwa hakika unasababishwa na mseto wa maambukizi'' alikariri Mbeki .

Rais huyo Mstaafu alisema mwaka wa 2006 kuwa HIV ndio inayosababisha vifo zaidi ya maradhi yote mengine nchini Afrika Kusini.

Kifuo kikuu ndio uliokuwa ukiorodheshwa wa pili wakati huo.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 73 hakuomba msamaha na kuwaudhi sana wanaharakati wa haki za kibinadamu ambao walidai msimamo huo tata ulikuwa wa kupotosha na kuwa ungesababisha maambukizi mengi zaidi na hatimaye vifo.