Mwanafunzi aliyemtishia Trump kuondoka Marekani

Elsayed Haki miliki ya picha AP
Image caption Elsayed alihojiwa na makachero wa Marekani mapema mwezi Februari

Mwanafunzi wa urubani kutoka Misri aliyeandika kwenye Facebook kwamba ulimwengu unaweza kumshukuru sana akimuua Donald Trump ameamua kuondoka Marekani kwa hiari.

Emadeldin Elsayed, 23, hakufunguliwa mashtaka yoyote ya uhalifu lakini maafisa wa Marekani walitaka afurushwe, wakili wake Hani Bushra amesema.

Maafisa wa hamiaji wamesema anaweza kuruhusiwa arejee nyumbani salama na kwa hiari mradi tu awe ameongoka kufikia tarehe 5 Julai.

Kwa sasa Elsayed anazuiliawa katika jela moja jimbo la California baada ya viza yake kufutiliwa mbali.

Bw Bushra alisema Jumatatu kwamba Elsayed anazuiliwa kinyume cha sheria.

“Anazuiliwa, nafikiri, kwa sababu yeye ni Mwislamu na mtu kutoka Mashariki ya Kati,” Bw Bushra aliambia shirika la habari la AP.

“Kijana huyu ataanza kutumiwa katika mabango ya kuichukia Marekani.”

Bw Elsayed alihojiwa na makachero wa Marekani mapema Februari baada yake kupakia picha ya Bw Trump kwenye Facebook na kuandika kwamba ako radhi kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kumuua bilionea huyo na kwamba ulimwengu unaweza kumshukuru kwa hilo, Bw Bushra alisema.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Trump alikuwa amependekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani

Bw Elsayed alikuwa awali amesema kwamba hakukusudia kumdhuru yeyote.

Alisema aliandika hayo kutokana na matamshi ya Bw Trump kuhusu Waislamu.

Bw Trump alikuwa mwisho mwa mwaka jana amependekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani.