ILO: Wanawake bado wanahangaika kazini

Wanawake Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wanawake wakiwa kazini

Utafiti wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) umeonesha hakuna hatua kubwa zilizopigwa katika kupunguza pengo kati ya wanawake na wanaume katika ajira duniani miongo miwili iliyopita.

Shirika hilo linasema pengo la ukosefu wa ajira kati ya wanawake na wanaume limepungua kwa asilimia 0.6 pekee tangu 1995.

Katika nchi ambazo wanawake hupata kazi kwa urahisi, bado kuna tatizo la kiwango na ubora wa kazi hizo.

Matokeo hayo ya utafiti yametolewa huku ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Mkuu wa ILO Guy Ryder, akizindua ripoti hiyo ya utafiti, amesema hilo ni dhihirisho kwamba wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kupata ajira.

"Katika umri wao wa kufanya kazi, wanawake wanaendelea kukubana na matatizo katika kupata kazi nzuri,” shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema.

"Ni hatua chache sana zilizoptwa tangu … 1995.”

Ripoti hiyo ilitathmini takwimu kutoka nchi 178 na kugungua kwamba kiwango cha kushirikishwa kwa wanawake katika ajira ni 25.5% chini ya kiwango cha wanaume mwaka 2015, kiwango hicho kikiwa kimeimarika kwa 0.6% kutoka miaka 20 awali.

Ripoti hiyo inasema asilimia 6.2 ya wanawake hawana kazi duniani wakilinganishwa na asilimia 5.5 upande wa wanaume.

Aidha wanawake wanaendelea kufanyikwa kazi saa nyingi kwa siku kwa jumla kuwashinda wanaume ukilinganisha na malipo kwa kazi iliyofanywa.

Urusi inaongoza duniani kwa kuwa na wanawake wengi nyadhifa kuu, ikifuatwa na Ufilipino na Lithuania.

Haki miliki ya picha Binita Dahal
Image caption Katika maeneo mengi duniani, wanawake hufanya kazi za nyumbani

Nchini Japan, ni 7% pekee ya nyadhifa kuu za uongozi ambazo zinashikiliwa na wanawake.

Kuna pia tofauti kubwa katika biashara kati ya wanaume na wanawake.

Ripoti hiyo inasema nchini Uganda na Tanzania, wanawake wengi wajasiriamali wamekuwa wakilalamikia gharama kubwa ya kusajili biashara na pia viwango vya juu vya ushuru kama moja ya sababu zinazowafanya kutosajili biashara zao.

Kadhalika, jamaa zao wakiwemo waume zao na mashemeji huwashauri kutorasmisha biashara zao.