China yaonywa na Marekani kuhusu visiwa

Image caption Visiwa vinavyopiganiwa na Uchina

Marekani imeonya kuwa mpango wa Uchina, wa kuanza safari za ndege za raia hadi kisiwa chenye mzozo, katika bahari ya Kusini ya Uchina, unaweza kuzidisha hofu baina ya nchi katika kanda, zinazodai eneo hilo.

Msemaji wa wizara ya mashauri ya nchi za nje ya Marekani, alieleza kuwa Uchina inafaa kufuata ahadi ilizotowa awali, kuonyesha uvumilivu na iache kupanua visiwa na miamba inayodhibiti.

Nchi kadha za Asia, pamoja na Malaysia, Ufilipino na Vietnam, piya zinadai visiwa hivyo.

Hapo jana shirika la habari la taifa, Xinhua, liliarifu kuwa safari za ndege za kusafirisha raia hadi mji wa Sansha, katika kisiwa cha Woody, zitakuwa zimeshaanza kabla ya mwaka mmoja kumalizika.