Syria: Al Nusra yapora washirika wa Marekani

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Syria: Al Nusra yapora washirika wa Marekani

Kundi la wapiganaji wa Syria, la Nusra, lenye ushirikiano na Al Qaeda, limeshambulia kundi linalosaidiwa na mataifa ya magharibi, katika jimbo la Idlib.

Kundi ambalo ni tawi la kundi linalojiita Jeshi Huru la Syria, linasema kuwa ofisi yao imevamiwa, na silaha kuibiwa, katika mji wa Maarat al-Numan.

Mapigano hayo yalizuka baada ya maandamano ya kupinga serikali, yali-po-geuka na kuanza kupinga kundi la Nusra, ambalo halimo katika makubaliano ya sasa ya kusitisha mapigano.

Nusra imebadilisha msimamo, na sasa inapigana dhidi ya makundi iliyokuwa inashirikiana nayo.

Wakati huohuo, Waziri wa Mashauri ya nchi za nje wa Marekani, John Kerry, ameionya serikali ya Syria isijaribu kuchafua mazungumzo ya amani.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waziri wa Mashauri ya nchi za nje wa Marekani, John Kerry, ameionya serikali ya Syria isijaribu kuchafua mazungumzo ya amani.

Hapo jana, waziri wa mashauri ya nchi za nje wa Syria, Walid al-Moallem, alisema ujumbe wa serikali utakwenda Geneva, kwenye mazungumzo yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa, yanayotarajiwa kuanza kesho, lakini alisema hakutakuwa na mazungumzo kuhusu uchaguzi wa rais.

Lakini akizungumza baada ya kukutana na mawaziri wengi wa mataifa ya Magharibi, Bwana Kerry aliionya serikali ya Syria na wasaidizi wake, wasichukue hatua zinazoweza kuvunja usitishwaji wa mapigano.