Amnesty: Buhari awaadhibu wanajeshi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Amnesty: Rais Buhari anastahili kuwaadhibu wanajeshi
Amnesty International pamoja na mashirika na wanaharakati wengine wa kutetea haki za binaadamu leo wameandaa maombi nje ya balozi za Nigeria kote duniani kutoa heshima kwa mamia ya wafungwa wanaotuhumiwa kuuawa na jeshi la Nigeria kwa usaidizi wa makundi ya vijana yanayowaunga mkono katika eneo la Maiduguri Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo takriban miaka 2 iliyopita.

Mauaji hayo yanafuata shambulio la Boko Haram dhidi ya kambi ya kijeshi Giwa ambako washukiwa wa mapigano ya kijihadi walikuwa wanazuiwa.

Shirika la Amnesty limesema kuwa limeandaa maandamano hayo kuadhimisha miaka miwili tangu raia mia sita arubaini (640) ambao walikuwa wakizuliwa na maafisa wa ulinzi waliuawa,

Shirika hilo limesema wengi wa waliouawa kwa kupigwa risasi ni wanaume na wavulana huku baadhi yao wakiuawa kwa kukatwa koo.

Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za kibinadamu limetaja kitendo hicho kama uhalifu wa kivita na kutoa wito kwa serikali ya Nigeria kuchunguza tukio hilo na kuwawajibisha wote waliohusika. Na ili kuhakikisha kuwa idadi kubwa ya watu wanafuatilia maandamano yaoi shirika hili limeanzisha ukarasa maalum kwenye mtandao Giwa640, hii ikiwa na maana ya kumbukumbu ya eneo walikouawa na idadi.

Machi 14 2014 wapiganaji wa Boko Haram walishambulia kambi ya jeshi iliyoko katika eneo la Giwa na kuwaachilia huru wanachama wake waliokuwa wamekamatwa pamoja na washukiwa wengine.

Image caption Kambi ya Boko Haram iliyoteketezwa

Hata hivyo maafisa wa jeshi la serikali waliwakamata washukiwa wengine waliojaribu kutoroka na waliuawa wakiwa chini ya ulinzi wa serikali.

Jeshi la Nigeria na wapiganaji wengine watiifu kwa serikali wamekuwa wakipambana na wapiganaji wa Boko Haram kwa zaidi ya miaka sita, katika maeneo ya Kaskazini mashariki mwa nchi

hiyo na mara nyingi wametuhumiwa kuhusika na ukiukwaji wa haki za kibinadam na mashirika ya kutetea haki a kibinadam yametaka wanajeshi hao kufungulia mashtaka.

Jeshi la nchi hiyo na wizara ya ulinzi haijasema lolote kuhusiana na maandamano hayo.