Erdogan aapa kukabili vikali magaidi

Erdogan Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rais Erdogan ameapa kuwakabili vikali magaidi

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameapa kwamba atawakabili vikali magaidi baada ya shambulio la kigaidi kuua watu zaidi ya 36 mjini Ankara.

Bw Erdogan amesema shambulio hilo lililotekelezwa kupitia gari lililotegwa mabomu litazidisha kujitolea kwa maafisa wa usalama wa Uturuki.

Mlipuko huo ulitokea katika kituo muhimu cha uchukuzi cha Guven Park na kujeruhi zaidi ya watu 100. Mshambuliaji mmoja anadaiwa kuuawa.

Waziri wa mambo ya ndani Efkan Ala alisema uchunguzi utakamilishwa Jumatatu na kwamba wote waliohusika watatajwa.

Hakuna kundi lililokiri kuhusika lakini duru za serikali zinashuku chama kilichopigwa marufuku cha Kurdistan Workers Party (PKK).

Waasi wa Kikurdi wametekeleza msururu wa mashambulio nchini Uturuki miezi ya karibuni na kuua mamia ya watu tangu kumalizika kwa mkataba wa kusitisha vita mwaka jana.

Kundi la Islamic State pia limetekeleza mashambulio Ankara karibuni.

Image caption Watu 36 waliuawa kwenye shambulio hilo

Uturuki inashiriki katika mashambulio yanayotekelezwa na majeshi yanayoongozwa na Marekani dhidi ya IS na huruhusu ndege za kivita za muungano huo kutumia kambi yake ya ndege ya Incirlik kutekeleza mashambuli Iraq na Syria.

Pia imekuwa ikishambulia ngome za wapiganaji wa Kikurdi wa People's Protection Units (YPG) kutoka Syria, ambao imekuwa ikisema ni sehemu ya PKK.

Bw Erdogan kupitia taarifa amesema makundi ya kigaidi yanawalenga raia kwa sababu yanashindwa vitani na majeshi ya Uturuki.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Serikali ya Uturuki inayatuhumu wakundi ya Kikurdi

Amehimiza kuwepo kwa umoja wa kitaifa lakini akasema Uturuki itatumia haki yake ya kujilinda kuzuia mashambulio siku zijazo.

"Watu wetu hawafai kuwa na wasiwasi, tutashinda vita hivi dhidi ya ugaidi na tutaangamiza ugaidi,” akasema.

Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali nchini Uturuki, Waziri Mkuu Ahmet Davutoglu ameahirisha ziara yake ya Jordan kutokana na shambulio hilo.