Chombo chatumwa kutafuta uhai Mars

ExoMars Haki miliki ya picha AFP
Image caption Chombo hicho kinatarajiwa kufika Mars Oktoba

Wataalamu wa anga za juu wa Ulaya kwa ushirikiano na wenzao wa Urusi wamerusha angani chombo cha anga za juu kitakachofanya utafiti kubaini iwapo kuna uhai sayari ya Mirihi, kwa Kiingereza Mars.

Chombo hicho kwa jina ExoMars Trace Gas Orbiter (TGO), kimepaa kutoka Baikonur nchini Kazakhstan saa 09:31 GMT.

Chombo hicho kitafanya uchunguzi kubaini iwapo gesi ya Methane ambayo imepatikana katika anga ya sayari hiyo inatokana na shughuli ya kijiolojia au inatokana na viumbe hai.

Mambo yote yakienda ilivyopangwa, wataalamu wanapanga baadaye kurusha mtambo wa kusafiri juu ya sayari, kwa kimombo rover, ambao utatumiwa kuchimba chini ya ardhi ya Mars.

Mtambo huo, utaunganishiwa nchini Uingereza, unaweza kurushwa mwaka 2018 au ukichelewa mwaka 2020.

Inakadiriwa kwamba itachukua roketi iliyobeba chombo cha TGO saa 10 ili kujiweka kwenye njia sahihi ya kuelekea sayari ya Mars.

Safari ya chombo hicho hadi Mars inatarajiwa kuchukua miezi saba, na sehemu ya chombo kwa jina Schiaparelli inatarajiwa kutua Mars tarehe 19 Oktoba. Sehemu ya setilaiti ya chombo hicho itazunguka sayari hiyo ikikusanya maelezo muhimu kuhusu hewa na gesi zinazopatikana katika sayari hiyo.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Setilaiti ya ExoMars

Safari ya chombo hicho inafuatiliwa na wataalamu wa Shirika la Anga za Juu la Ulaya mjini Darmstadt, Ujerumani.

Mradi huo wa TGO ndio wa kwanza kabisa kufanywa na Ulaya na Urusi kwa pamoja kuelekea sayari ya Mars, ambayo ndiyo ya nne kutoka kwenye jua.

Uchunguzi wa awali wa setilaiti zinazozunguka dunia na rover ya Curiosity ya Marekani umebaini kuwepo kwa haidrokaboni ingawa za vipimo vya chini sana katika sayari hiyo.

Moja ya mambo yanayoweza kuwa yanachangia kuwepo kwa gesi hizo ni shughuli za kijiolojia ndani ya sayari hiyo ambapo maji yanaweza kuwa yanachanganyikana na mawe na kuzalisha gesi ya haidrojeni ambayo baadaye inageuka na kuwa methane.

Jambo jingine linaloweza kuwa linasababisha kuwepo kwa gesi hiyo ni kuwepo kwa viumbe hai.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Sehemu ya chombo hicho kwa jina Schiaparelli ndiyo itakayotua Mars

Sehemu kubwa ya gesi ya methane duniani hutokana na viumbe hai.