Maskini aliyewafichua watoro kulipwa $100,000

Hay Haki miliki ya picha AP
Image caption Hay-Chapman alikuwa ameona picha za wawili hao kwenye runinga

Mwanamume asiye na makao kutoka San Francisco katika jimbo la California nchini Marekani atazawadiwa $100,000 (£71,000) kwa kuwasaidia polisi kuwakamata wafungwa waliokuwa wametoroka jela.

Matthew Hay-Chapman aliona picha za wafungwa hao watoro kwenye runinga na akafanikiwa kuwatambua wakiwa kwenye gari walilokuwa wameiba.

Wawili hao walikuwa wametoroka jela ya Orange County siku sita awali na walikuwa wametafutwa sana.

Zawadi kamili ya $150,000 (£106,000) itawaendea watu wane, lakini Bw Hay Chapman ndiye atakayepata sehemu kubwa.

Wafanyakazi wawili wa duka la jumla la Target watapokea $15,000 (£11,000) kila mmoja kwa kupiga ripoti kwa polisi baada ya kuwaona wanaume wawili waliowashuku kwenye ukanda wa kamera za usalama.

Mwanamume mkazi wa Los Angeles aliyepokonywa gari na wawili hao naye atapokea $20,000 (£14,000).

Bw Hay-Chapman aliwaona watoro hao wakiwa kwenye gari hilo karibu na duka moja San Francisco na akawapasha habari maafisa wa usalama wa eneo hilo.

Wafungwa hao Hossein Nayeri na Jonathan Tieu walikamatwa muda mfupi baadaye.