Ashtakiwa kwa kuiba picha za utupu za watu maarufu

Haki miliki ya picha thinkstock
Image caption Mdukuaji

Mtu mmoja ameshtakiwa kwa kudukua akaunti za kampuni ya Apple icloud na akaunti za Gmail za watu maarufu pamoja na kuiba picha na kanda zao za utupu.

Mamlaka ya Marekani imesema kuwa Ryan Collins amekiri kufanya kosa hilo.

Waendesha mashtaka wamependekeza kwamba akabiliwe na kifungo cha miezi 18 jela ,ijapokuwa jaji ana uwezo wa kuongeza kifungo hicho na kufikia miaka 5.

Mtu huyo mwenye umri wa miaka 36 amedaiwa kuiba majina ya akaunti pamoja na nywila.

Idara ya haki imesema kuwa Collins anayetoka katika jimbo la Pennsylvania amekiri kuvunja na kuingia katika zaidi ya akaunti 100 kati ya mwezi Novemba mwaka 2012 na Septemba 2014.

Amedaiwa kufanikiwa katika udukuzi huo baada ya kuwatumia barua pepe waathiriwa zilizodai kutoka kwa Google ama Apple zikitaka majina ya akaunti hizo pamoja na nywila zao.

Collins ameshtakiwa kwa kudukuwa akaunti 59 za icloud na akunti yengine 72 za Gmail.