Wapiganaji 30 wa al-Shabab wauawa Somalia

al-Shabab Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiganaji wa al-Shabab wamekuwa wakitekeleza mashambulio ya mara kwa mara Somalia

Maafisa wa serikali ya Somalia na jeshi la Kenya wamesema wapiganaji 30 wa al-Shabaab wameuawa katika mashambulio mawili tofauti.

Maafisa wa serikali katika jimbo la Puntland wanasema wapiganaji 11 waliuawa walipojaribu kushambulia viji kadha katika pwani ya nchi hiyo.

Jeshi la Kenya nalo linasema wapiganaji 19 waliojaribu kushambulia kambi ya majeshi hayo katika mji wa Afmadhow, kusini mwa Somalia.

Gavana wa mkoa wa Nugal katika jimbo la Puntland, ambako mapigano yalitokea, alisema wapiganaji wengi wa al-Shabaab walijaribu kushambulia pwani ya Puntland.

Mapigano makali yalishuhudiwa zaidi mji wa Garmaal.

Mashambulio yao yalianza mapema asubuhi ambapo walikabiliana vikali na wanajeshi wa Puntland.

Jeshi la Kenya nalo lilisema wapiganaji walijaribu kushambulia kambi za wanajeshi wa Kenya na Somalia usiku wa kuamkia Jumatano lakini wakakabiliwa vikali karibu na mji wa Afmadhow.

Wapiganaji 19 waliuawa na bunduki kumi aina ya AK47 kupatikana pamoja na guruneti 3 za kurushwa kwa kutumia roketi.