ANC: Hata Zuma anaweza kuchukuliwa hatua

Zuma

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Rais Zuma anadaiwa kudhibitiwa na familia ya Gupta

Katibu Mkuu wa chama tawala cha African National Congress (ANC) amesema hakuna asiyeweza kuchukuliwa hatua chama, akiwemo Rais Jacob Zuma, shirika la habari la Reuters linaripoti.

Matamshi ya Gwede Mantahse yametokea baada ya Naibu Waziri wa Fedha Mcebisi Jonas kufichua kwamba aliahidiwa kazi ya waziri wa fedha na familia yenye ushawishi mkubwa ya Gupta.

Familia hiyo imekanusha tuhuma hizo.

Bw Zuma anakabiliwa na shinikizo kutokana na madai ya mara kwa mara kuhusu uhusiano wake na familia ya Gupta, ambayo imekuwa ikituhumiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za nchi hiyo.

Rais huyo anatarajiwa kukabiliwa na maswali bungeni baadaye leo.

Mwezi uliopita, Bw Zuma alipokuwa akitoa hotuba yake ya hali ya taifa kwa bunge, wanachama wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) waliimba "Zupta must go!" [Zupta (Zuma na Gupta) sharti aondoke] kabla ya kufurushwa kutoka ukumbi wa bunge.

Mtandao wa habari wa News24 wa Afrika Kusini unaripoti kwamba chama cha upinzani cha Congress of the People kinajiandaa kuwasilisha mashtaka ya uhaini dhidi ya rais.