Ebola yarejea tena Guinea

Guinea

Chanzo cha picha, Reproducao BBC News

Maelezo ya picha,

Guinea ilitangazwa kutokuwa na Ebola miezi mitatu iliyopita

Watu wawili wamegunduliwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa Ebola nchini Guinea, karibu miezi mitatu tangu taifa hilo kutangazwa kutokuwa na ugonjwa huo.

Jamaa watatu wa watu hao wawili waliogunduliwa kuwa na Ebola walifariki hivi majuzi baada ya kuonesha dalili za virusi hivyo.

Visa hivyo viwili vimeripotiwa saa chache baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza kumalizika kwa mlipuko wa ugonjwa huo katika taifa jirani la Sierra Leone.

Hata hivyo, WHO imetahadharisha kwamba virusi hivyo vinaweza kujitokeza tena wakati wowote.

Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, ambao ndio mbaya zaidi katika historia, ulianza nchini Guinea 2013.

Watu zaidi ya 11,000 walifariki kutokana na ugonjwa huo Afrika Magharibi.