Wapiganaji wa al-Shabaab wazingirwa Somalia

Mapigano Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mapigano makali yamekuwa takiendelea tangu Jumatatu

Wapiganaji takriban 200 waliokuwa wameshambulia eneo moja katika jimbo la Puntland, wamezingira na wanajeshi wa jimbo hilo.

Naibu rais wa jimbo hilo Abdihakim Amry ameambia BBC kwamba wanajeshi hao wamewapa wapiganaji hao agizo la kuwataka kujisalimisha la sivyo wakabiliwe.

Mapigano makali yamekuwa yakiendelea katika eneo hilo la Suuj, ambalo linapatikana katika mkoa wa Nugaal katika pwani ya jimbo hilo lililo na uhuru kiasi kutoka kwa Somalia.

Wapiganaji wa al-Shabaab walifika eneo hilo kwa boti na kuchukua udhibiti.

Wanajeshi watano wa Puntland wanaripotiwa kuuawa kwenye mapigano na wanamgambo hao katika eneo hilo.

Jana, kituo cha redio cha kibinafsi cha Radio Mustaqbal kilimnukuu Naibu Waziri Mkuu wa Somalia Mohamed Omar Arte akisema serikali kuu iko tayari kutuma wanajeshi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika (Amisom) “kukabiliana na wapiganaji hao wa al-Shabab eneo la Puntland iwapo watahitajika”.