Utafiti: Elimu huwafaidi wezi pia

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Utafiti: Elimu huwafaidi wezi pia !

Wasomi ambao wamegeukia wizi kama njia ya kujichumia riziki hupata fedha nyingi kuwazidi wezi ambao sio wasomi.

Utafiti uliofanya na chuo kikuu cha Essex nchini Uingereza kwa ushirikiano na kile cha California nchini Marekani umebaini hayo.

Watafiti hao kutoka Uingereza na Marekani waliwachunguza viongozi na wanachama zaidi ya 400 wa magenge kadha yaliyotuhumiwa kwa kutekeleza wizi katika miaka ya 1940- 1960.

Magenge hayo yalihusishwa na kundi la Mafia lenye asili ya Italiano na mizizi yake nchini Marekani.

Watafiti walibaini kuwa wanachama wa magenge waliosalia vyuoni kwa mwaka mmoja zaidi walipata mapato zaidi ya wale ambao hawakusoma zaidi.

Uwezo wa kutathmini haraka hesabu uliwapa takriban asilimia 8% zaidi ya mapato.

Na kwa wale wezi walioshiriki katika visa vya ulghai, na kughushi stakabadhi muhimu za serikali mapato yao yaliimarika kwa zaidi ya asilimia 16% kumzidi mwananchi mtiifu wa sheria ambaye alikwenda shuleni kwa mwaka zaidi ya mwizi.

Kwa ufupi mwizi aliyeelimika alipata faida na pesa maradufu ya mwenzake ambaye aliamua kuchapa kazi na kujitafutia mkate wake wa kila siku kwa njia halali.

Je ,hapo ulipo ukiwatizama watuhumiwa wa wizi walaghai na hata matapeli unakubaliana na utafiti huu ?

Toa maoni yako na uyachapishe kwenye mtandao wetu wa Facebook Twitter Instagram : Tafuta #BBCSwahili