Magufuli ahakiki bunduki zake mbili

Magufuli Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania
Image caption Rais Magufuli akiitoa bastola yake ihakikiwe

Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli ametoa bunduki zake mbili aina ya shortgun na pistol na zikahakikiwa nyumbani kwake ikulu jijini Dar es salaam.

Kiongozi huyo ndiye mtu kwanza kutekeleza agizo la mkuu wa mkoa wa Dar es salaam la kuhakiki silaha, kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu.

Uhakiki wa silaha hizo umefanywa na maafisa wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Simon Sirro.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Rais Magufuli ametoa wito kwa watu wote wanaomiliki silaha nchini humo kuhakikisha zinahakikiwa.

Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania

Aidha, amelitaka jeshi la polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ili kutokomeza kabisa vitendo hivyo.

"Ni aibu kumuona askari polisi mwenye silaha ananyang'anywa silaha, ni aibu, na nasema hiyo ni aibu, mpaka jambazi akunyang'anye silaha na wewe una silaha?" amesema Dkt Magufuli.