Israeli yawaokoa wayahudi Yemen

Haki miliki ya picha
Image caption Israeli yawaokoa wayahudi Yemen

Israel imesema kuwa imewaokoa wayahudi wa mwisho waliokuwa wamekwama katika taifa lililoko katika lindi la vita la Yemen.

Watu 19 kutoka miji ya Sanaa na Raydah, wamesafirishwa kwa ndege hadi Israeli baada ya vikosi vya kijeshi vya Israeli kutekeleza operesheni ya siri.

Halmashauri ya Wayahudi ambayo huwajibika katika operesheni za kuwarejesha nyumbani wayahudi kote duniani ,inasema kuwa mmoja kati ya wale waliorejeshwa nyumbani ni rabbi (mwalimu wa dini) ambaye alikuwa amebeba Torah (maandiko ya kidini) yaliyokisiwa kuwa yamedumu kwa zaidi ya miaka 500.

Licha ya juhudi zao, takriban wayahudi 50 waliamua kusalia nchini humo.

Tangu mwaka wa 1948, Wayahudi 51,000 wamehamia Israeli kutoka Yemen ambayo ndio iliyokuwa na kizazi kilichodumu zaidi cha wayahudi.

Haki miliki ya picha Arielle DiPorto para La Agencia Judia para Israel
Image caption Watu 19 kutoka miji ya Sanaa na Raydah, wamesafirishwa kwa ndege hadi Israeli

Asilimia kubwa yao walipelekwa Israeli katika operesheni kubwa na ya siri ya Operation Magic Carpet kati ya mwaka wa 1949 na 1950.

Katika miaka ya hivi karibuni asilimia kubwa ya wayahudi waliokuwa wakiishi Yemen wamekabiliwa na mashambulizi huku taifa hilo likiisambaratika na vita.