Uber: Rais wa Indonesia akwama kwenye foleni

Image caption Maelfu ya waendeshaji na wamiliki wa magari ya uchukuzi pikipiki na tuktuk wameziba mabarabara Jakarta

Rais wa Indonesia Joko Widodo leo alinaswa katika maandamano makubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini humo dhidi ya kampuni inayotoa huduma za teksi kupitia kwa mtandao wa Intaneti Uber.

Maelfu ya waendeshaji na wamiliki wa magari ya uchukuzi pikipiki na tuktuk waliungana na kuziba mabarabara ya kuingia na kutoka kati kati ya jiji la Jakarta.

Image caption Wahudumu hao walikuwa wanaitaka serikali izipige marufuku huduma za teksi na uchukuzi za Uber na Grab

Wahudumu hao walikuwa wanaitaka serikali izipige marufuku huduma za teksi na uchukuzi za Uber na Grab wakidai kuwa inawanyima kitega uchumi kutokana na bei yao ya chini wanayotoza wateja wao.

Waandamanaji hao waliwashambulia waendeshaji teksi wengine ambao hawakuwa wanashiriki katika mgomo huo.

Mgomo huo awali ulikuwa umeitishwa na waendeshaji teksi ambao ndio walioathirika pakubwa na kuja kwa Uber.

Image caption Abiria waliopanda pikipiki walishambuliwa

Hata hivyo leo walipokuwa wakiandamana waliungwa mkono na wapinzani wao wakuu yaani wandesha Bajaj au TukTuk mbali na madereva wa magari ya uchukuzi wa umma.

Kama ilivyotokea katika mataifa mengine yote madereva hao wanadai kuwa japo serikali zinasisitiza kuwa huduma ya teksi ya Uber imeruhusiwa kufanya biashara yake kihalali, waendeshaji wake hawajagharamia vyeti vingi kama walivyogharamika wenyewe kupata vibali vya kuendesha biashara hiyo ya uchukuzi.

Waandamanaji waliziba mabarabara yote yanayoelekea bungeni, afisi ya mkuu wa jiji la Jakarta ,wizara ya mawasiliano mbali na maeneo yenye maofisi mengi kati jiji hilo.

Haki miliki ya picha Bhayu Sugarda
Image caption Waandamanaji hao waliwashambulia waendeshaji teksi wengine ambao hawakuwa wanashiriki katika mgomo huo.

Dereva mmoja wa teksi aliyekuwa akishiriki katika mgomo huo Salahuddin,anasema kuwa ''wao wanatozwa kodi nayo Uber inaruhusiwa kuendesha biashara yao wakitumia magari ya kibinafsi''

''Naandamana kwa sababu ya haki ya kujichumia inadhulumiwa na hawa mabepari wanaokuja na kutunyang'anya kazi zetu'' aliongezea kusema .

Ahmad Rahoyo ambaye ni mhudumu wa Bajaj anasema kuwa

Image caption Waendeshaji Bajaj walijiunga na mgomo huo

''Kabla ya kuja kwa Uber nilikuwa napata takriban Rupia laki moja kila siku ,hiyo ni sawa na dola $10, lakini sasa hata kugharamia mafuta imekuwa tatizo"

Serikali ya Indonesia imeshindwa kutoa mwongoza mahsusi kutokana na misimamo inayokanganya umma.

kwa upande mmoja wizara ya uchukuzi inawaunga mkono waendeshaji magari ya teksi na Bajaj kuwa programu hizo za uchukuzi (Uber na Grab) zipigwe marufuku.

Image caption Tuktuk

Kwa upande wake rais Joko Widodo anapinga kwa kinywa kipana kuwa programu hizo za teknolojia ya mawasiliano haifai kupingwa bali kukumbatiwa na mikono mwili la sivyo uchumi wa Indonesia itaachwa nyuma.

Sawa na Uber, Grab yenye makao yake makuu nchini Malaysia inawaruhusu wateja wa pikipiki za uchukuzi kugawana nauli na hivyo imepingwa kwa kupunguza gharama na hivyo kazi za vijana wanaotegemea pikipiki au Bodaboda kujichumia riziki.