Brussels: Polisi wasaka mshukiwa ‘aliyenusurika’

Ubelgiji Haki miliki ya picha AFP
Image caption Raia Ubelgiji walikesha wakiomboleza waliofariki

Polisi nchini Ubelgiji wanamsaka mshukiwa anayedaiwa kuhusika katika mashambulio yaliyotekelezwa mjini Brussels Jumanne na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 30.

Mwanamume huyo alionekana akitembea pamoja na washukiwa wengine wawili uwanja wa ndege wa Zaventem kabla ya milipuko miwili kutokea.

Washukiwa wenzake wawili walifariki katika mashambulio hayo baada ya kujilipua, mwendesha mashtaka wa Ubelgiji amesema.

Misako ya kuwasaka magaidi imefanywa maeneo mbalimbali Ubelgiji.

Kundi linalojiita Islamic State (IS) limedai kuhusika.

Taarifa iliyopakiwa mtandaoni na kundi hilo ilisema maeneo hayo yaliyoshambuliwa “yaliteuliwa kwa umakinifu mkubwa” na kuonya kuwa kutatokea mabaya zaidi kwa mataifa yanayopinga kundi la Islamic State.

Wizara ya mashauri ya kigeni ya Marekani imewataka raia wake wanaosafiri Ulaya wachukue tahadhari.

“Makundi ya kigaidi yanaendelea kupanga mashambulio ya kuteketelezwa karibuni kote Ulaya, yakilenga hafla za michezo, maeneo ya kitalii, migahawa na uchukuzi,” taarifa ya wizara hiyo ilisema.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Picha ya mshukiwa anayesakwa na polisi

Mwendesha mashtaka wa Ubelgiji Frederic Van Leeuw amesema polisi wanamtafuta mwanamume aliyeonekana amevalia kofia na jaketi la rangi isiyokolea sana.

Amesema misako inaendelea katika maeneo mbalimbali nchini humo na kwamba kilipuzi chenye misumali, kemikali na bendera ya IS vilipatikana katika nyumba moja eneo la Schaerbeek, Brussels.

Msako huo wa Schaerbeek ulitekelezwa baada ya dereva wa texi aliyewasafirisha washukiwa hao watatu hadi uwanja wa ndege kuwapasha polisi habari.

Meya wa Zaventem Francis Vermeiren, ameambia AFP kwamba washukiwa walitekeleza mashambulio uwanja wa ndege kupitia mabomu yaliyotegwa kwenye mabegi yao.

Saa moja baada ya milipuko uwanja wa ndege, mlipuko mwingine ulitokea kituo cha treni cha Maelbeek karibu na makao makuu ya EU.

Haijabainika shambulio hilo lilitekelezwa vipi lakini IS wamesema kwamba hata hilo lilikuwa shambulio la kujitoa mhanga.

Maafisa wa Ubelgiji wamesema idadi ya watu waliofariki mashambulio yote mawili ni zaidi ya 30, 11 wakifariki uwanja wa ndege na 20 kituo cha treni.

Watu karibu 250 walijeruhiwa, wengi wao vibaya.