Mahakama yawaachia huru washukiwa wa Mpeketoni

Haki miliki ya picha ODPP
Image caption Dyna Salim na Mahadi Swaleh walikuwa wakikabiliwa na mashtaka sitini ya mauaji

Mahakama ya Mombasa nchini Kenya imewaachilia huru washukiwa wawili wa mauaji ya Mpeketoni, Lamu kwa ukosefu wa ushahidi.

Washukiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya watu sitini huko Mpeketoni miaka miwili iliyopita.

Mahakama imesema uchunguzi duni ulifanyika.

Watu 60 waliuawa katika mashambulizi yaliyotekelezwa usiku wa Juni miaka miwili iliyopita.

Image caption Watu 60 waliuawa katika mashambulizi yaliyotekelezwa usiku wa Juni miaka miwili iliyopita.

Subira ya miaka miwili kungoja haki itendeke imetumbukia nyongo kwa wahanga wa mauaji ya Mpeketoni yaliyodaiwa kutekelezwa na wapiganaji wa Al Shabab.

Washukiwa wakuu wa mojawapo ya mauaji ya kikatili zaidi nchini Kenya wako huru tena, na mahakama imewalaumu polisi kwa utepetevu.

Dyna Salim na Mahadi Swaleh walikuwa wakikabiliwa na mashtaka sitini ya mauaji, lakini mahakama haikupata ushahidi wa kutosha kuwahukumu.

Hakimu Martin Muya alisema polisi walishindwa kudhibitisha bila shaka kuwa washukiwa hao walihusika na mauaji hayo.

Image caption Hakimu huyo alitaja kuvurugika kwa mawasiliano kwenye kikosi cha polisi wakati wa mauaji.

Aidha alisikitika kuwa rasilimali nyingi zilitumika kwenye uchunguzi huo, huku akitaja uchunguzi uliofanywa na maafisa wa polisi kuwa hafifu.

Huku akitoa uamuzi wake, hakimu Muya aliitaka serikali ya Kenya kushughulikia wasiwasi za kiusalama.

Hakimu huyo alitaja kuvurugika kwa mawasiliano kwenye kikosi cha polisi wakati wa mauaji.

Alisema hakukuwa na mawasiliano mema baina ya vikosi vilivyokuwa Mpeketoni, wala mwongozo mwema kutoka Nairobi.

Image caption Hakimu Martin Muya alisema polisi walishindwa kudhibitisha bila shaka kuwa washukiwa hao walihusika na mauaji hayo.

Pia aliwakosoa polisi kwa kusita kuwaokoa waathiriwa usiku wa manane kwa kuogopa kufumaniwa na wavamizi hao.

Kwa muda sasa polisi wameikashifu idara ya mahakama kwa kutoimarisha vita dhidi ya ugaidi, wakidai eti washukiwa huachiliwa huru kwa urahisi.

Lakini uamuzi huu umerudisha ngoma upande wa polisi, ambao ni jukumu lao kuwakamata washukiwa na kukusanya ushahidi wa kutosha kuhakikisha wamefungwa jela.