Afrika Kusini kufukua miili 83 ya mashujaa

Haki miliki ya picha THINKSTOCK
Image caption Afrika Kusini kufukua miili 83 ya mashujaa

Waziri wa sheria wa Afrika Kusini ametangaza kuwa mabaki ya wafungwa 83 wa kisiasa walionyongwa na serikali ya makaburu yatafukuliwa.

Wote walinyongwa wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Maiti zao zilizikwa katika ardhi ya jela ambayo zamani ilifahamika kama gereza la Pretoria.

Mabaki hayo yatatambuliwa kisha kupewa familia zao ili yazikwe upya.

Wengi wa wafungwa hao walikuwa wanachama wa vyama vya Pan Africanist Congress-(POQO) na United Democratic Front-UDF.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wizara ya maswala ya haki na sheria nchini humo inasema kuwa takriban wafungwa wa kisiasa na mashujaa 130 walinyongwa katika gereza hilo la Pretoria

Vyama hivyo ndivyo vilivyohusika pakubwa katika vuguvugu la kupinga utawala wa weupe waliokuwa wachache kwa pamoja na chama cha African National Congress -ANC kilichoongozwa na Nelson Mandela.

Awali mabaki ya wafungwa wengine 47 yalifukuliwa kisha kuzikwa upya.

Wizara ya maswala ya haki na sheria nchini humo inasema kuwa takriban wafungwa wa kisiasa na mashujaa 130 walinyongwa katika gereza hilo la Pretoria kati ya mwaka wa 1960- na 1990.