Waziri wa Kenya 'azuiwa' bandari ya Tanga

Lamu Haki miliki ya picha Kenya Ports Twitter
Image caption Ujumbe kutoka Kenya na Uganda ulikuwa ukikagua bandari za Lamu, Mombasa na Tanga

Waziri wa Kawi wa Kenya Charles Keter na maafisa wengine wakuu Kenya walizuiwa na maafisa wa Tanzania kuingia bandari ya Tanga, gazeti la Daily Nation la Kenya limeripoti.

Kisa hicho kilitokea Jumatano kwa mujibu wa gazeti hilo.

Inadaiwa kwamba maafisa wa Tanzania walimpokonya Bw Keter pasipoti yake pamoja na pasipoti za maafisa wa Kenya walioandamana naye punde baada ya kuwasili.

Maafisa hao walikuwa wameandamana na maafisa kutoka Uganda kukagua bandari ya Tanga kama sehemu ya mashauriano ambayo yanaendelea kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta.

Maafisa wa Uganda hata hivyo hawakuzuia kuendelea na safari hiyo.

Tanzania na Uganda ziliafikiana kuhusu ujenzi wa bomba hilo kutoka bandari ya Tanga hadi Uganda na majuzi Rais Magufuli aliagiza ujenzi wa mradi huo uharakishwe.

Lakini mwaka jana, Uganda na Kenya zilikuwa zimeanza mashauriano kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta la kutoka bandari ya Lamu.

Nchi hizo hata hivyo hazikukamilisha mazungumzo.

Baada ya Tanzania na Uganda kuafikiana, wakati wa ziara ya Rais Museveni nchini Tanzania, Rais Uhuru Kenyatta alimwalika Rais Museveni kwa mashauriano jijini Nairobi ambayo yalifanyika ikulu ya Nairobi Jumatatu wiki hii.

Taarifa iliyotumwa na Bw Keter baada ya mkutano huo ilisema viongozi hao waliafikiana kukutana wiki mbili zijazo mjini Kampala kwa mashauriano zaidi.

Iliafikiwa pia kwamba makundi ya wataalamu kutoka nchi zote mbili yalainishe habari kuhusu mpango bora zaidi wa kujenga bomba la mafuta kwa gharama nafuu, changamoto katika ujenzi, kuthibitisha hazina ya mafuta iliyopo na kulinganisha bandari za Lamu, Mombasa na Tanga.

Kabla ya kuelekea Tanzania, maafisa hao walikuwa wametembelea bandari ya Lamu katika pwani ya Kenya.

Gazeti la Daily Nation linasema maafisa hao wa Kenya walirejeshewa pasipoti zao baada ya saa moja hivi.