Wanahabari wawili mashuhuri washtakiwa Uturuki

Novemba Haki miliki ya picha epa
Image caption Dundal na Gul walikamatwa mwezi Novemba

Wanahabari wawili wamashuhuri nchini Uturuki watafunguliwa mashtaka ya kufichua siri za serikali.

Can Dundar na Erdem Gul, waliokuwa wakifanyia kazi gazeti la Cumhuriyet, walikamatwa Novemba baada ya kuchapishwa kwa taarifa zilizodai kwamba serikali ya Uturuki ilijaribu kusafirisha silaha kwa wapiganaji wa Kiislamu nchini Syria.

Wanakanusha mashtaka hayo lakini wanakabiliwa na kifungo cha maisha jela iwapo watapatikana na hatia.

Wafuasi wa wanaume hao wawili wanasema kesi hiyo ni mtihani mkuu kwa uhuru wa uanahabari nchini Uturuki.

Serikali ya Uturuki imekosolewa sana kimataifa ikidaiwa kuwahangaisha wanahabari.

Mapema mwezi huu, polisi wa Uturuki walivamia afisi za gazeti kubwa nchini humo, Zaman, saa chache baada ya uamuzi wa mahakama kuipa serikali uhuru wa kuchukua udhibiti wa gazeti hilo.

Can Dundar alikuwa mhariri mkuu wa gazeti la Cumhuriyet naye Erdem Gul alikuwa mkuu wa afisi ya gazeti hilo mjini Ankara.

Walikamatwa mwezi Novemba mwaka jana.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Gazeti la Cumhuriyet huunga mkono upinzani

Rais Recep Tayyip Erdogan aliwasilisha malalamishi dhidi yao yeye binafsi.

Walizuiliwa kwa muda kabla ya kesi yao kuanza lakini wakaachiliwa Februari baada ya Mahakama ya Kikatiba kuamua kuwa haki zao za uhuru na kujieleza vilikiukwa.