Zaidi ya 70 wafa kwa mlipuko Pakistani

Haki miliki ya picha AFP

Zaidi ya watu 70 wamekufa na wengine kujeruhiwa katika mlipuko uliotokea kwenye eneo la wazi la kupumzikia lenye shughuli nyingi katika mji wa Lahore nchini Pakistan.

Polisi wanasema mlipuaji mwenye kujitoa mhanga alijilipua karibu na eneo la kuchezea watoto mahali wazazi walipokuwa wamejikusanya ambao baadhi yao walikuwa wakisherehekea siku kuu ya Pasaka.

Wengi ya waliokufa na kujeruhiwa katika tukio hilo ni watoto. Tayari kundi la Taliban la Pakistan la Jamaat ul Ahrar limekiri kuwa ndilo linalohusika na shambulizi hilo. Msemaji wa kundi hilo amesema walikusudia kuwalenga jamii ya wakristo waliopo katika mji huo.

Haki miliki ya picha AFP

Afzal ni mmoja ya wakazi wa mji wa Lahore yeye alikuwa ni miongoni mwa waliosaidia kuwasaidia majeruhi baada ya mlipuko kutokea.

" Nimewabeba zaidi ya watoto ishirini ambao walipelekwa hosptalini. Nilisaidia kubebe miili mitatu na kupakia kwenye gari la polisi. Wakati mlipuko ulipokuwa unatokea watoto walikuwa wakicheza kwenye uwanja huo wa wazi. Leo jamii ya wakristo walimaliza mfungo na kusherehekea Pasaka. Wakristo wengi walifika hapa katika tukio hili. Siwezi kuelezea jinsi tukio hilo la kusikitisha lilivyokuwa."

Naye Tariq Fatimi ambaye ni mshauri wa Waziri Mkuu wa Pakistani ameiambia BBC kuwa tukio hilo ni la kinyama bila kujali ni nchi gani imelengwa.

" Hata kama shambulizi hilo limetokea Peshawar au Lahore au Brussels au Paris au London, Sisi sote tunapaswa kuwa pamoja kwa sababu huu ni uhalifu ambao hauathiri nchi moja pekee, au jamii moja lakini inaathiri wanadamu wote."